KAHAMA FM KWA KUSHIRIKIANA NA WADAU WA MISITU WAPANDA MITI 300 SHULE YA MSINGI NYAHANGA A NA MBULU


Na Samwel Nyahongo
KAHAMA.

Ukosefu wa elimu juu ya umuhimu wa upandaji miti kwa ajili ya uhifadhi wa Mazingira miongoni mwa wakazi wa wilaya ya KAHAMA Mkoani SHINYANGA imekua ni changamoto na kusababisha baadhi ya maeneo wilayani humo kukabiliwa na hatari ya kuwa jangwa.

Hayo yamesemwa na Mmoja wa Wadau wa Maendeleo wilayani humo, Bibi ASHA MSANGI (NAKYOO), katika uzinduzi wa kampeni ya upandaji kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani uliofanyika katika Shule za Msingi Nyahanga “A” na Mbulu mjini Kahama.

SANJARI na kuhimiza elimu ya mazingira kwa Wananchi, MSANGI amesema vyombo vya dola havina budi kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha vitendo vyovyote vya uharibifu wa mazingira vinakomeshwa wilayani humo na katika taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake Mkuu wa shule hiyo BERNADETHA MLWANGWA ameishukuru Kahama fm pamoja na wadau wote walioshiriki kwa kuiona shule hiyo kwani changamoto ya kukosekana kwa miti katika shule yake ni kubwa.

Amewahakikishia Wadau mbalimbali waliohudhuria uzinduzi wa kampeni hiyo wakiwemo Wawakilishi wa Wakala wa Misitu nchini (TFS), Umoja wa Wapanda Miti Kahama na Chama Kikuu cha Ushirika Wilaya ya Kahama (KAKU), kwamba watahakikisha miti yote iliyopandwa inatunzwa na kukua.

Katika hatua nyingine MLWANGWA ameiomba mamlaka ya mji safi na usafi wa mazingira mjini Kahama (KUWASA) kuwapunguzia bei ya bili ya maji ili waweze kupata unafuu katika umwagiliaji wa miti hiyo.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Nyahanga MICHAEL MAGILE amewaomba wananchi kutunza mazingira na kuacha kuharibu miundombinu hali ambayo itapunguza magonjwa ikiwemo magonjwa ya mlipuko.

Jumla ya miti 300 inatarajiwa kupandwa katika shule hizo za Msingi za Nyahanga “A” na Mbulu katika maadhimisho hayo ya Siku ya Mazingira Duniani nchini ya kampeni hiyo yenye kauli mbiu isemayo: OTESHA MITI-KAHAMA YA KIJANI INAWEZEKANA.

Siku ya Mazingira Duniani huadhimishwa kila Juni Tano ya kila Mwaka ambapo kimataifa kauli mbiu yake inasema: TOKOMEZA UCHAFUZIWA MAZINGIRA UNAOSABABISHWA NA MIFUKO MICHAFU YA PLASTIKI.

Kitaifa maadhimisho hayo yamefanyika katika viwanja vya Mnazi mmoja jijini Dar es salaam ambapo kaulimbiu ya kitaifa ni MKAA UNA GHARAMA, TUMIA NISHATI MBADALA.
Share:

No comments:

Post a Comment

IDADI YA WASOMAJI

TUSIKILIZE LIVE KUPITIA TUNEIN

UNGANA NASI FACEBOOK HAPA

10 ZILIZOSOMWA ZAIDI

Labels