SERIKALI: WAANDISHI WA HABARI ACHENI KUCHANGANYA TAALUMA NA SIASA

SERIKALI imewataka waandishi wa habari nchini kutochanganya taaluma zao na ushabiki wa siasa ili kuandika habari zenye tija katika jamii zenye kuleta maendeleo .
Wito huo umetolewa February 13 mjini Dodoma na naibu waziri wa Habari michezo na utamaduni Bi Juliana Shonza katika maadhimisho ya siku ya Redio duniani iliyofanyika kitaifa mjini Dodoma katika ukumbi wa Hotel ya Nasheera.
Akiongea kwa niaba ya waziri wa habari Dr Harrison Mwakyembe,Bi Shonza amesema waandishi wa habari wanapoingia kwenye siasa,hawatoandika habari za mizania hali itakayoleta migogoro katika jamii.
Katika hatua nyingine Bi shosa ametoa wito kwa waandishi wa habari kudumisha mila na desturi hasa katika matumizi ya fasaha ya Lugha ya Kiswahili na kusema kuwa kwa sasa waandishi na watangazaji wengi wanatumia lugha ya Kiswahili na kuchanganya na lugha ya kingereza kwa wakati mmoja.
Naye Katibu wa Mtadao wa Radio Jamii (TADIO), Marco Mipawa akisoma hotuba kwa niaba ya Mwenyekiti wa mtandao huo, Prosper Kwigize alitaka serikali kuhakikisha kwamba urasimu unaondolewa kwenye utoaji wa taarifa kwa umma ili kuwezesha kufanyika kwa vipindi mbalimbali vya habari. 
Alitaka Tamisemi kuweka utaratibu wa utoaji habari katika mfumo rahisi ili wananchi wafahamu kinachotekelezwa na serikali yao. Aidha maafisa habari walioajiriwa wapewe mamlaka na wawezeshwe kufahamu kinachofanywa na serikali na wawe na ruhusa ya kutoa taarifa kwa vyombo vya habari katika maeneo yao.
Aidha alisema kutokana kutokuwa na vyanzo vya mapato ya uhakika serikali ingeangalia suala la kodi na ushuru mbalimbali ili kusaidia Redio za Jamii kutolipia huduma za Radio.
Pia amesema sheria zilizopo ukilinganisha na mazingira halisi ya kazi ya mwanahabari, mfano sheria ya Takwimu, sheria ya huduma za habari, sheria ya makosa ya mtandao kumeshabibisha tasnia ya habari na utangazaji kuwa katika mashaka zaidi kuliko kipindi kilichopita. 
Ameongeza kwa kuiomba  Serikali kutoa Ruzuku ya elimu au mafunzo ya kitaaluma kwa wanahabari ili kuwawezesha kukidhi vigezo vya kisheria ifikapo 2021.
Awali akitoa salamu za Shirika la umoja wa mataifa la Elimu,Sayansi na Utamaduni-UNESCO- Kiongozi mkuu wa ofisi ya Shirika hilo Dar es salaam Bi Faith Shayo ametoa wito kwa waandishi wa habari kuandika habari za Usawa wa kijinsia,Maendeleo na zenye kudumisha amani.
Siku ya redio duniani huazimishwa kila mwaka tarehe 13 mwezi wa 2 duniani Pote na kauli mbiu ya mwaka huu ni Redio na michezo.
MATUKIO KATIKA PICHA:  

 
Katibu wa Mtandao wa Radio za Jamii nchini (TADIO), Marco Mipawa akisoma hotuba kwa niaba ya Mwenyekiti wa Mtandao huo, Prosper Kwigize wakati maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani yaliyofanyika mjini Dodoma kwa ufadhili wa UNESCO.
 

 
 
 
Kaimu Mkuu wa Ofisi za Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) nchini, Faith Shayo (wa pili kushoto) akitoa salamu za UNESCO wakati maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani ambapo huadhimishwa kila mwaka tarehe 13 Februari yaliyofanyika mjini Dodoma na kuhudhuriwa na waandishi wa habari wa vyombo vya habari vya jamii kutoka Tanzania Bara na Visiwani pamoja na wadau wengine wa habari nchini. Kutoka kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mheshimiwa Dkt. Binilith Mahenge, Mgeni rasmi Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mh. Juliana Shonza (wa pili kulia) pamoja na Mkuu wa Mawasiliano na Habari wa Tume ya Taifa ya Unesco (NATCOM), Christina Musaroche (wa kwanza kushoto).
 
 
Mkuu wa Mawasiliano na Habari wa Tume ya Taifa ya Unesco (NATCOM), Christina Musaroche akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Kaimu Katibu Mtendaji wa tume hiyo Dk. Moshi Kimizi (hayupo pichani) wakati wa maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani yaliyofanyika Mjini Dodoma.
 
 
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mheshimiwa Dkt. Binilith Mahenge akizungumza machache kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mh. Juliana Shonza wakati wa sherehe za maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani yaliyofanyika mjini Dodoma.
 
 
Mgeni rasmi Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mh. Juliana Shonza akiwasili katika hoteli ya Nashera mjini Dodoma kushiriki sherehe za maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani akiwa ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mheshimiwa Dkt. Binilith Mahenge (kulia) pamoja na Katibu wa Mtandao wa Radio za Jamii nchini (TADIO), Marco Mipawa (kushoto).
 
Kutoka kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mheshimiwa Dkt. Binilith Mahenge, Mgeni rasmi Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mh. Juliana Shonza, Kaimu Mkuu wa Ofisi za Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) nchini, Faith Shayo pamoja na Mkuu wa Mawasiliano na Habari wa Tume ya Taifa ya Unesco (NATCOM), Christina Musaroche wakiwa meza kuu wakati wa sherehe za maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani mjini Dodoma.
 
Mratibu wa Mtandao wa Vyombo vya Habari na Jinsia Kusini mwa Afrika (GEMSAT) , Gladness Munuo akitoa mada kuhusu usawa wa jinsia katika kuripoti michezo, changamoto na taratibu zake wakati wa sherehe za maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani yaliyofanyika mjini Dodoma.  
Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena akisisitiza umuhimu wa maudhui katika vipindi vya redio ambapo aliwaasa kutangaza masuala yanayowahusu wanajamii katika maeneo yanayohusika badala ya kuwalisha wasikilizaji taarifa ambazo ziko nje na mipaka wanayoishi.
 
Mtaalamu wa Vyombo vya Habari na Mawasiliano, Mariagoreth Charles akiwasilisha kanuni za uandishi wa habari za mtandaoni na mitandao ya kijamii kwa waandishi wa habari wa vyombo vya habari vya jamii kutoka Tanzania Bara na Visiwani pamoja na wadau wengine wa habari nchini walioshiriki kwenye maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani yaliyofanyika mjini Dodoma.
 
Mtangazaji Mkongwe wa Habari za Michezo nchini, Abdallah Majura amesema pamoja na kwamba waandishi wanatangaza vipindi vya michezo lakini maudhui hayakidhi na kuvutia vile inavyostahili akitoa mfano hai wakati akichangia kwa nini waandishi wengi hawaandiki habari za michezo. Majura amesema yeye mwenyewe amewahi kupata tuzo mbili kwa ajili ya vipindi vya michezo.
 
Pichani juu na chini ni sehemu ya waandishi wa habari wa vyombo vya habari vya jamii kutoka Tanzania Bara na Visiwani pamoja na wadau wengine wa habari nchini waliohudhuria sherehe za maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani yaliyofanyika mjini Dodoma.
 
Mgeni rasmi Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mh. Juliana Shonza (wa tatu kushoto), Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mheshimiwa Dkt. Binilith Mahenge (kushoto) pamoja na Kaimu Mkuu wa Ofisi za Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) nchini, Faith Shayo (wa tano kulia) wakicheza wimbo maalum wa ngoma za asili wa Kikundi cha Kaza Roho cha mjini Dodoma ulioongozwa na Msanii Mwinamila wakati wa sherehe za maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani yaliyofanyika mjini Dodoma.
 
Mgeni rasmi Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mh. Juliana Shonza na meza kuu wakiwa katika picha ya pamoja na waandishi wa habari wa vyombo vya habari vya jamii kutoka Tanzania Bara na Visiwani pamoja na wadau wengine wa habari nchini wakati wa sherehe za maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani yaliyofanyika mjini Dodoma.
Share:

No comments:

Post a Comment

IDADI YA WASOMAJI

TUSIKILIZE LIVE KUPITIA TUNEIN

UNGANA NASI FACEBOOK HAPA

10 ZILIZOSOMWA ZAIDI

Labels