Waziri wa Kilimo Ashuhudia Hafla Ya Utiaji Saini Mikataba Ya Ubanguaji Korosho Tani 7500

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) jana Tarehe 10 Januari 2019 ameshuhudia hafla ya utiaji saini mikataba ya ubanguaji korosho kati ya Bodi ya nafaka na Mazao Mchanganyiko Tanzania na wenye viwanda vya ndani.

Mkurugenzi wa Bodi ya nafaka na Mazao Mchanganyiko Tanzania Dkt Hussein Mansoor ndiye ametia saini kwa niaba ya serikali na Kampuni nne zimesaini mikataba ya awali kuanza kazi hiyo ambazo ni kampuni ya Hawte Investment Co. Ltd, Micronix Mtwara, Korosho Afrika, na Micronix-Newala.

Kampuni hizo zimeingia mikataba ya Jumla ya Tani 7500 ambapo kampuni ya Hawte Investment Co. Ltd yenye uwezo wa kubangua Tani 2000 kwa mwaka imesaini mkataba wa Tani 1500.

Kampuni ya Micronix ya mjini Mtwara yenye uwezo wa kubangua Tani 2400 kwa mwaka imeingia mkataba wa Tani 1200. Kampuni ya Korosho Afrika ya Mjini Tunduru Mkaoni Ruvuma yenye uwezo wa kubangua Tani 5000 kwa mwaka imeingia mkataba wa kubangua Tani 2400 ilihali Kampuni ya Micronix ya Wilayani Newala yenye uwezo wa kubangu Tani 5000 kwa mwaka imeingia mkataba wa kubangua Tani 2400.

Akizungumza katika hafla hiyo ya utiaji saini Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) amesema kuwa serikali imepitia vifungu vyote vya kisheria kabla ya kuanza kuingia makubaliano na kampuni hizo kwa ajili ya ubanguaji wa Korosho.

Alisema kuwa zoezi la ubanguaji tayari lilikuwa limeanza kupitia Shirika la Kushughulikia viwanda vidogo vidogo (SIDO) ambalo tayari limeajiri wafanyakazi 160.

Alisema kuwa Shirika la Kushughulikia viwanda vidogo vidogo (SIDO) pamoja na majukumu mengine lakini lilikuwa na kazi mbili ambazo ni kuhakikisha wanatengeneza vipuli na mashine mbalimbali ambazo zimeharibika. Vileviele kuhamasisha wabanguaji wadogo wadogo na kuwasajili.

“Baada ya kuwasajili mtatakiwa kuingia nao mikataba kwa kiasi cha korosho wanachokihitaji kwa ajili ya ubanguaji” Alikaririwa Mhe Hasunga

Mhe Hasunga alisema kuwa serikali ina matumaini makubwa kuwa mikataba ya ubanguaji iliyosainiwa itazingatiwa kwa kufuata taratibu na masharti yote kwa mujibu wa sheria.

Alisisitiza kuwa serikali inaingia mikataba na viwanda ambavyo vimekuwa vikibangua kwa muda mrefu hivyo haina mashaka na ubora wa ubanguaji.

Aidha, Alisema kuwa viwanda hivyo vitakuwa na uhakika wa kufanya kazi usiku na mchana kutokana na malighafi nyingi iliyopo tofauti na miaka iliyopita ambapo malighafi ilikuwa haipatikani kutokana na korosho kubanguliwa nje ya nchi.

Mhe Hasunga amesisitiza kuwa serikali imeamua kubangua korosho zote nchini ili kuongeza wigo wa ajira kwa wananchi sambamba na kuongeza thamani ya korosho inayozalishwa nchini ili iweze kuuzwa kwa jina la Tanzania. Ambapo Wizara ya Kilimo itaweza kuchangia kwa ufasaha katika uchumi wa nchi.

Share:

Naibu Waziri Aweso Atoa Onyo Kali Kwa Mkandarasi Muleba

Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso ametoa onyo kali kwa Mkandarasi anayefanya kazi ya ujenzi wa Mradi wa Maji Katoke, Wilaya ya Muleba DC, mkoani Kagera baada kubaini changamoto mbalimbali katika mradi huo.

Mradi huo ambao umegharimu kiasi cha zaidi ya Shilingi milioni 476, umeonekana kuwa na kasoro mbalimbali licha ya kukamilika kwake, jambo lililomfanya Naibu Waziri kukasirishwa na Mkandarasi.

Naibu Waziri Aweso amemtaka Mkandarasi huyo awepo kwenye eneo la mradi, atakapofika kuukagua mradi huo, ambaye licha ya kuandikiwa barua tano zikimtaka kufanya marekebisho, bado amekuwa hafiki eneo la mradi na kufanya marekebisho stahiki.

Amesema ni lazima mkandarasi huyo afike na kueleza ni kwanini mradi huo una matatizo, pamoja na kuwa umekamilika unakosa thamani halisi ya fedha (value for money) zilizotumika kujenga mradi huo.

Ikibainika kuna ubadhirifu wa fedha hatua kali zitachukuliwa ikiwemo kuwafukuza wote kazi Mkandarasi na Mhandisi wa Wilaya, pamoja na kuwafikisha katika vyombo vya sheria kwa ajili ya kuchukuliwa hatua.

“Niwaonye watendaji wa Sekta ya Maji, hakikisheni mnawapa kazi wakandarasi wenye uwezo ambao watafanya kazi nzuri na kisha kuidai Serikali malipo yao; sio wakandarasi wajanja ambao wamekuwa wakila fedha za Serikali kiholela bila matokeo kuonekana”, alionya Aweso.

“Ndio maana nimefika Kagera kujionea fedha ambazo wizara inazitoa kama zinaleta matokeo na sio kuchezewa, huku kilio cha wananchi cha huduma ya majisafi na salama kikiendelea. Jambo hilo halina nafasi  kwenye Serikali ya Awamu ya Tano na Wizara ya Maji kwa sasa”, alisisitiza Aweso.

Akatoa tahadhari kwa kusema kuwa tunapoelekea kuanzisha Wakala wa Maji Vijijini (RUWA) wahandisi wababaishaji hawatakuwa na nafasi. Wizara itahakikisha inafanya utaratibu wa kuhakiki uwezo wa wahandisi wote wa maji na kuondoa wazembe na wanaokosa uadilifu.

Naibu Waziri Aweso atakua ziarani Kagera kwa siku tano kukagua miradi ya maji na kutatua changamoto.
Share:

Nguo zinazofanana na sare za JWTZ zanaswa kambi ya wakimbizi Kigoma

Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma, imekamata nguo zinazofanana za sare za kijeshi katika makambi ya wakimbizi.
 
Akizungumza na waandishi na kamati hiyo mjini hapa jana Alhamisi Januari 10, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Samson Hanga, alisema nguo hizo zilikamatwa Desemba 31 mwaka jana kati ya saa tano asubuhi hadi sita mchana kwenye  makambi ya wakimbizi.

“Jumla ya nguo zinazofanana na sare za kijeshi 1,947 zilikamatwa katika kambi ya wakimbizi ya Mtendeli na Nduta zote za hapa hapa Kigoma.

“Katika Kambi ya Nduta zilikamatwa sare 1,325 na Mtendeli 622,” alisema.

Pamoja na mambo mengine, alisema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea ili kuwabaini walioingiza sare hizo na lengo lao.
Share:

Wahukumiwa Miaka 7 Jela Kwa Kuchezesha Upatu na utakatishaji fedha.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu Jones Moshi na James Gatuni, kulipa faini ya Sh milioni 204 au kwenda jela miaka saba kwa kosa la kuendesha biashara ya upatu na utakatishaji fedha.

Waliohukumiwa ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Rifaro Africa Ltd, Jones Moshi (42) mkazi wa Mbezi Beach Dar es Salaam na Mkurugenzi mwenza wa Kampuni hiyo, James Gatuni (35) raia wa Kenya.

Akisoma hukumu hiyo Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, alisema katika kosa la kwanza la utakatoshaji fedha watu kila mmoja anatakiwa kulipa faini ya Sh milioni mbili na endapo watashindwa kufanya hivyo watatakiwa kutumikia kifungo cha miaka miwili gerezani.

Mashauri alisema katika shtaka la pili linalohusu utakatishaji fedha haramu kila mshtakiwa atatakiwa kulipa faini ya Sh milioni 100 na endapo atashiwa kufanya hivyo atalazimika kutumikia kifungo cha miaka mitano jela.

“Lakini wakishindwa kulipa faini za makosa yote watatakiwa kutumikia kwenda gerezani kama adhabu kwa makosa yote mawili” alisema Mashauri.

Awali Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro, akisaidiana na Wakili Esther Martine na Neema Mbwana alidai mahakamani hapo kuwa wawili hao walitenda kosa hilo kati ya Julai 14 mwaka 2014 na March 31 mwaka 2016, jijini Dar es Salaam na maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Share:

Ajali ya Hiace Yaua Watu Wawili

Watu  wawili wamefariki dunia papo hapo baada ya gari aina ya Totota Hiace walilokuwa wamepanda kuacha njia na kupinduka.

Kamanda wa Polisi mkoani Rukwa, George Kyando, alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi majira ya alasiri. Aliwataja watu waliofariki katika ajali hiyo ni Augenia Masumbuko (53) mkazi wa Isale, na Nestory Kayumba mkazi wa Kalambo.

Kamanda huyo alisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni dereva aliyekuwa akiendesha gari lenye namba za usajili T 795 CVA aina ya Toyota Hiace kushindwa kulimudu katika mteremko, hivyo kuacha njia na kupinduka.

Katika ajali hiyo watu wawili pia walijeruhiwa ambao ni Akoba Kung'ombe (40) mkazi wa Bangwe na mwingine ambaye hajafahamika ambaye ni mwanaume mwenye umri kati ya miaka 25-30.

Kamanda Kyando alisema miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika kituo cha afya Namanyere, na majeruhi wamelazwa katika Zahanati ya Myula kwa ajili ya matibabu.

Kwa mujibu wa Kamanda Kyando, dereva wa gari hilo alikimbia baada ya ajali hiyo na kwamba Jeshi la Polisi linaendelea kumsaka ili afikishwe mahakamani.

Aliwaasa madereva mkoani humo kwa makini wawapo barabarani na kufuata sheria za usalama barabarani, ili kuepuka vifo na majeruhi kutokana na ajali zinazoweza kuepukika.
Share:

Lori Laigonga Treni Jijini Dodoma.....Watu Wawili Wajeruhiwa

Image result for ajali ya lori na treni
Watu wawili wamenusurika kifo baada ya lori aina ya scania walilokuwa wakisafiria kutoka Dodoma kwenda Iringa kuigonga treni ya mizigo katika makutano ya reli na barabara eneo la hazina jijini Dodoma.

Tukio hilo lilitokea jana mchana mara baada ya lori hilo lenye namba za usajili T463 ADW likiwa na tela lenye usajili T483 BLP kuiigonga treni hiyo iliyokuwa ikitoka jijini Dar es salaam kuelekea mikoa ya kanda ya ziwa.

Baadhi ya mashuhuda wa ajali hiyo wamesema kuwa ajali hiyo imechangiwa na mvua zilizokuwa zikinyesha na kumfanya dereva wa lori kutoona kizuizi cha treni mbele yake.

Mmoja wa mashuhuda hao Ramadhani Rashid Mkazi wa Majengo amesema kuwa ajali hiyo ilichangiwa na dereva wa lori kutaka kukatiza kwa mwendo mkali lakini alikuwa kacheleWa hali iliyosababisha kugongwa na treni hiyo ya
mizigo.

“Dereva wa lori alikuwa katika mwendo mkali wakati akikatiza kivuko cha reli hivyo alishindwa kusimama na treni likawa limekaribia na kumgonga tumetoa watu wawili wakiwa wamejeruhiwa vibaya mwingine mmoja utumbo ukiwa nje”alisema

Kaimu kamanda wa polisi mkoani Dodoma ACP William Mkonda, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema chanzo ni uzembe wa dereva wa lori ambaye kwa sasa anashikiliwa na polisi na majeruhi wamelazwa katika hosipitali ya rufaa ya mkoa wa Dodoma
Share:

Rais Magufuli amtaka Waziri Mpya wa Madini Dotto Biteko kuanzisha vituo vya madini mikoa inayofanya shughuli za uchimbaji

Rais John Magufuli amemwagiza Waziri wa Madini, Dotto Biteko kuanzisha vituo vya madini kwenye maeneo yanayozalisha migodi nchini.

Alitoa maagizo hayo baada ya kuwaapisha viongozi wapya wa serikali jana  Jumatano, Ikulu jijini Dar es Salaam. 

Rais Magufuli alieleza kuwa maagizo hayo yanalenga kudhibiti madini yanayoibwa na kupelekwa nje huku nchi kushindwa kunufaika ipasavyo.

“Ripoti mbalimbali katika nchi za Afrika Mashariki zinaonyesha Tanzania kuwa nyuma katika uuzaji wa dhahabu wakati sisi ndio tunaongoza katika uchimbaji, kwa ripoti hii ni lazima tujiulize tunakwama wapi? Dhahabu tunazochimba zinauzwa wapi? Soko lipo wapi na tunalijua? Tunapouza tunapata fedha kiasi gani? Wizara ipo na wataalamu wake na hapo ndio changamoto inapoonekana” Alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli aliagiza pia Waziri Biteko kushirikiana na Benki Kuu (BOT) kuweka mkakati utakaowezesha nchi kuanza kununua dhahabu na kuitunza. 

“Tanzania lazima isimame, hatuwezi kuendelea kuibiwa dhahabu, lazima tutunze dhahabu yetu, itatufaa hata shilingi yetu ikishuka,” aliongeza.

Share:

Mzee wa Miaka 80 Auawa na Kunyofolewa Sehemu zake za Siri

Watu wawili wamefariki  dunia mkoani Kagera katika matukio mawili tofauti, likiwamo la mzee mmoja aliyejulikana kwa jina la Laurian Kakoto (80), mkazi wa kijiji cha Ihunga kata Kishanda wilayani Muleba, kukatwa sehemu zake za siri na wahusika kuondoka nazo.

Akizungumza na waandishi wa habari, kamanda wa polisi mkoani Kagera Revocatus Malimi amesema kuwa baba huyo aliondoka nyumbani Januari 7 mwaka huu kwenda kuhemea lakini hakurudi hadi maiti yake ilipogunduliwa na wananchi ikiwa imezikwa huku nyayo za miguu zikiwa zinaonekana juu ya kaburi, Januari 08 saa moja asubuhi.

Kamanda Malimi amesema kuwa baada ya wananchi kugundua tukio hilo walitoa taarifa polisi, ambapo walifika na kufukua mwili huo uliokuwa umezikwa kwa kutanguliza kichwa chini, na kukuta amekatwa kwa kitu chenye ncha kali shingoni na sehemu za siri.

Aidha kamanda huyo amesema kuwa jeshi la polisi linaendelea kuwasaka wananchi waliojichukuliwa sheria mkononi kwa kuchoma moto nyumba 16 na kufyeka migomba, mali za watu waliowatuhumu kumuua mwendesha bodaboda mmoja Albert Antipas, aliyetoweka tangu Januari 02 mwaka huu na maiti yake kupatikana ikiwa katika bwawa la kufugia samaki, Januari 07.

Amesema kuwa maiti ya mwendesha bodaboda huyo ilikutwa ikiwa imefungwa kwa kamba mikononi na miguuni, na kisha kufungwa katika jiwe na kuzamishwa katika bwawa hilo. 

Baada ya wananchi wa kijiji cha Kibingo tarafa ya Murongo wilayani Kyerwa kusikia kuwa watuhumiwa wamekamatwa na polisi, ndipo walipokwenda kuchoma moto nyumba zao.
Share:

Rais Magufuli Akerwa na Viongozi Anaowateua Kuanza Kugombana Badala ya Kufanya Kazi

Rais John Magufuli ameweka wazi kwamba hafurahishwi na migogoro kati ya viongozi anaowateua na kusema kuwa amewaweka kiporo Mkuu wa Wilaya  na Mkurugenzi wake kutokana na matendo yao ya kugombana badala ya kufanya kazi hivyo wasifikiri kwamba hafahamu.
 
Rais Magufuli ameyasema hayo jana baada ya kumaliza kuapisha viongozi wapya aliowateua baada ya kufanya mabadiliko katika Wizara mbalimbali pamoja na Makatibu wa Wizara.

Rais alisema kwamba anafahamu changamoto ni nyingi katika utendaji wa kazi ingawa yapo mengine mazuri wanayofanya na kuwataka wahakikishe wanajitoa kwa maslahi ya wananchi.

"Nafahamu hizi kazi zina changamoto nyingi sana mfano kuna DC Gairo na Mbunge hawaelewani mpaka Mbunge anapost kumtukana DC tena mke wa mtu, hajui kama anaweza upoteza Ubunge, "I hope' siku moja ataomba msamaha kwenye Bunge", alisema Mh Rais Magufuli na kuongeza;

"Halmashauri ya Nyasa wanagombana sana DC na Mkurugenzi, nimewaangalia tu! nimewaachia kiporo chao. Pale Dodoma Mkurugenzi wa Jiji na DC walikuwa wanagombana nika-send meseji nikawaambia endeleeni kugombana siku moja mtagombania Vijijini, wamenyamaza naona yameisha".
Share:

Tume ya Taifa ya Uchaguzi DRC Yamtangaza Mshindi wa Kiti cha Urais...Tazama Hapa

Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Congo (Ceni) imetangaza matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo yanayoonesha mgombea wa upinzaniFelix Tshisekedi ameshinda kiti cha Urais katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Desemba 30 mwaka uliopita.
 
Tshisekedi amemshinda mgombea mwingine wa upinzani Martin Fayulu, pamoja na mgombea aliyekuwa anaungwa mkono na serikali ya Rais anayemaliza muda wake, Emmanuel Shadary.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Ceni) Corneille Nangaa, mapema leo Alhamisi amesema kwamba kwamba Bw Tshisekedi amepata asilimia 38.57 ya kura zilizopigwa na kumtangaza rasmi kuwa Rais mteule wa nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa madini na mafuta.

Tshisekedi anatokea katika muungano wa kisiasa na aliyekuwa mgombea wa chama cha UNC (Union for the Congolese Nation), Vital Kamerhe ambaye atakuwa ni Waziri Mkuu wa serikali yao kwa mujibu wa makubaliano yao.

Ripoti zinaeleza kuwa mshindi wa kwanza (Felix Tshisekedi) amepata kura takriban milioni 7, huku mshindi wa pili (Martin Fayulu akipata kura takriban milioni 6.4 milioni na mgombea wa tatu ambaye anaungwa mkono na Rais Joseph Kabila (Emmanuel Ramazani Shadary) akipata takriban kura millioni 4.4.
Share:

Waziri Mkuu Kuzindua Mashine 5 za X-ray zilizogharimu Bilioni 2.1

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa anatarajiwa kuzindua mashine tano za mionzi (X-ray) za kidigitali katika Hospitali za Rufaa za mikoa mitatu na mbili za wilaya.

Uzinduzi huo unatarajiwa kufanyika leo, Ijumaa katika Hospitali ya Ruvuma. Mashine zote zimeigharimu serikali jumla ya Sh bilioni 2.1.

Hospitali zilizofungiwa mashine hizo in pamoja na hospitali za rufaa za mkoa wa Morogoro, Simiyu na Ruvuma na Hospitali za halmashauri za wilaya ya Chato na Magu. 
Aidha, Hospitali nyingine tano za mikoa na moja ya halmashauri inaendelea kukamilisha ufungaji wake.
Share:

Lugola Ampa Siku 7 Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Kagera (RCO)


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, ametoa siku saba kwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Kagera (RCO), Obassy Nguvillan, kupeleleza upya kesi ya mama aliyechomewa nyumba katika eneo la Kyakailabwa Kata ya Nyanga, Manispaa ya Bukoba.

Lugola alitoa agizo hilo jana kutokana na watuhumiwa kukamatwa kisha kuachiwa na baadaye jalada kufungwa na Mwanasheria wa Serikali.

Kabla ya agizo hilo, mama huyo, Sauda Amir, alilalamika kwa Waziri Lugola katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Uhuru Manispaa ya Bukoba na baadaye RCO alikiri kuwa inawezekana Jeshi la Polisi lilipeleleza kesi hiyo kwa udhaifu.

Lugola alisema kuwa haiwezekani mwanamke huyo achomewe nyumba, watuhumiwa anawafahamu halafu kesi iishe katika mazingira ambayo yana utata na kulazimika kumwita RCO kujibu.

“RCO natoa muda wa wiki moja ufanye kazi hii wewe mwenyewe, uchunguze kesi hii upya na unipe majibu,” alisema.

Akizungumzia tukio hilo, Sauda anayedai alifiwa na mumewe, alisema kuwa nyumba yake ilichomwa moto Juni 11, mwaka jana na kuwa kutokana na tukio hilo, kwa sasa hana mahala pa kuishi.

“Mheshimiwa Waziri, naomba unisaidie suala langu lipatiwe ufumbuzi, nahangaika na watoto, sina pa kuishi, kwa sasa mimi na watoto wangu saba tumepewa hifadhi na mama mmoja katika eneo la Kyakailabwa,” Alisema mama huyo
Share:

Wamiliki Wa Nyumba za Kupanga Wapewa ONYO

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angeline Mabula, amewaonya baadhi ya watu wanaomiliki nyumba na kuendelea kuwatoza wapangaji wao kodi za miezi sita na mwaka mmoja, kinyume na maelekezo ya serikali, kuheshimu maelekezo hayo.

Naibu waziri huyo alitoa onyo hilo jana, alipokuwa akihojiwa na kituo kimoja cha redio na kuwataka wenye nyumba hao kuwasaidia mwananchi wa kawaida.

"Lengo na madhumuni ni kumsaidia Mtanzania wa kawaida ambaye hutegemea kipato cha mshahara ama biashara, ili aweze kufanya bajeti yake kama kulipa nyumba ama matumizi mengine. Unapomwambia alipe miezi sita ama mwaka mmoja unamtaka atafute kipato cha ziada akuridhishe mwenye nyumba halafu mpangaji abaki na madeni kitu ambacho hakimsaidii Mtanzania," alisema.

Alisema mkakati wa serikali ni kuweka vitu katika usawa ili kuwawezesha wapangaji.

Mabula alisema sheria kuhusu suala hilo bado haijatungwa, lakini ni vizuri wenye nyumba wakajiandaa mapema ili sheria itakapopitishwa wawe wameshazoea.

"Kwa sasa ipo katika mchakato haujapelekwa muswada wa kusomwa bungeni kwa kuwa bado hatujachukua maoni ya wadau, lakini ndani ya mwaka wa fedha unaokuja itakuwa tayari maana imeonekana ni hitaji kubwa," alisema.

Mwishoni mwa mwaka juzi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, aliagiza watu wanaomiliki nyumba za kuzipangisha, kuacha kuwatoza wapangaji wao kodi za miezi sita hadi mwaka mmoja ili wasio na uwezo waweze kumudu maisha.

Waziri Lukuvi, wakati akitoa agizo hilo, alisema mpangaji anatakiwa kulipa kodi kila mwezi labda atake mwenyewe kulipa kwa miezi zaidi ya mmoja.
Share:

Lugola Awataka Polisi Watafute Njia Mbadala ya Kuwakamata Bodaboda Badala ya Kuwavizia na Kusababisha Ajali


Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amewataka polisi kuja na njia mbadala za kuwakamata madereva bodaboda badala ya kuwavizia kwenye minada na magulio na kusababisha ajali.

Lugola amesema hayo jana Jumatano Januari 2, 2019 Bukoba mkoani Kagera katika mkutano wa hadhara.

Amesema hakuna ulazima wa kufukuzana na waendesha pikipiki kwa kuwa vyombo wanavyoendesha vinaweza kuchukuliwa namba kuliko kuwavizia na kufukuzana nao.

Ameonya hatua ya kuwavizia kwenye minada, magulio na maeneo mengine inawaathiri hata abiria wanaokuwa wamebebwa katika pikipiki hizo kwa kupata ajali.

Katika mkutano huo wa hadhara uliofanyika uwanja wa Mashujaa baadhi ya waendesha pikipiki wamedai hakuna mazingira rafiki ya kufanya kazi kati yao na Polisi.

Hata hivyo, Waziri Lugola amewataka waendesha pikipiki kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kulinda haki za watumiaji wengine wa barabara.
Share:

Dereva wa Lori la Mafuta Atiwa Mbaroni Kwa Kusafirisha Wahamiaji Haramu Songwe

Dereva wa lori la mafuta  Christopher Kikwete (42) mkazi wa Kibamba Jijini Dar es Salaam anashikiliwa na polisi mkoani Songwe kwa tuhuma za kusafirisha wahamiaji haramu 10 raia wa Ethiopia kinyume cha sheria.

Kamanda wa Polisi mkoani huo, Mathias Nyange amesema hayo jana Jumatano Januari 02, 2019 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Amesema dereva huyo alikamatwa Desemba 31, 2018 katika stendi ya mabasi ya Makaburini mjini Vwawa wilayani Mbozi saa 4 asubuhi wakati polisi kwa kushirikiana na Idara ya Uhamiaji wakiwa katika doria walilisimamisha lori hilo na kukuta limejaza wahamiaji hao katika kitanda kilichopo nyuma ya kiti cha dereva.

Kamanda huyo amesema lori hilo lenye namba T 500 DFJ na tera lenye namba T 833 CMN aina ya Scania ni tanki lililokuwa limebeba mafuta ya petroli kutoka Dar es Salaam kwenda nchini Zambia nalo linashikiliwa na jeshi hilo.
Share:

CCM Kuyefyekelea Mbali Majina ya Wagombea Watakaobainika Kutumia Rushwa


Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Dkt Bashiru Ally, amesema chama hicho hakitasita kuyakata majina ya wananchama wake ambao watabainika kutumia njia ambazo si halali ili kuhakikisha wanapewa nafasi ya kugombea uongozi kwenye chama hicho.
 
Dkt Bashiru ametoa kauli hiyo wakati akiwa kwenye ziara ya kikazi Mkoani Bukoba, ambapo alikutana na viongozi mbalimbali wa CCM, pamoja na viongozi wa vyama vya mazao.

"Ukifuatilia siasa za CCM wakati wa uchaguzi, ilikuwa ni za kutumia pesa, kununulia wanachama kadi, mfumo wa uteuzi umebadilika, kura za maoni watu wengi hawatahusika, si kwa sababu hawatakiwi kupata haki bali kutakuwa na mchujo utaosimamiwa vizuri," amesema Dk Bashiru.

Aidha kuelekeea Uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika mwaka huu, kiongozi huyo amewataka wananchi kutowachagua viongozi wanaowapa hela, kwakuwa uchaguzi wa serikali za mitaa ni uchaguzi muhimu kuliko uchaguzi mkuu kwa sababu serikali za mitaa ndizo zilizo karibu na wananchi na zinazogusa maisha ya kila siku ya wananchi.

"Tumeanza kuhamasisha wanachama wenye sifa waanze kujitokeza hasa sehemu za vitongoji na vijiji, kwasababu uchaguzi wa mwaka huu utakua ni uchaguzi wa wanachama wenye sifa, sio wanachama wanaoweza kufanya siasa za kutumia pesa au kupendeleana," ameongeza Dkt Bashiru.
Share:

Wanaoanza kidato cha kwanza mwaka huu watakiwa kwenda na kiti na meza

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Kayombe Lyoba amewaagiza wazazi na walezi wenye watoto wanaotarajia kujiunga kidato cha kwanza  mwaka huu kuhakikisha wanakwenda na kiti  na meza ili waweze kuingia darasani.

Hali hiyo imekuja baada ya halmashauri hiyo kuongeza kasi kwenye ujenzi wa vyumba vya madarasa ili kila mwanafunzi aliyechaguliwa kuingia kidato cha  kwanza  apate fursa ya kuanza masomo.

“Tunawaomba wazazi na walezi wawezeshe watoto wao kuja na kiti na meza pindi wanapokuja kuanza masomo Januari 7, kwani tayari tumeshaongeza jitihada kuhakikisha vyumba vya madarasa vinakuwepo vya kutosha ili asikose kuingia mwanafunzi hata mmoja,” alisema  Lyoba.

Alisema jumla ya wanafunzi 4,136 wamepokewa na halmashauri iwemeweza kujenga vyumba vya madarasa 87 na kubakiwa na upungufu wa vyumba 32.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Kibena Kingo alisema mbali na jitihada za kujenga maabara katika shule zao kuna changamoto ya uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi.

“Halmashauri yetu ina upungufu wa walimu 41 wa kufundisha masomo ya sayansi, hivyo tunamwagiza Ofisa Elimu Sekondari kulifuatilia suala hilo kwa ukaribu ili tuweze kuondokana na changamoto hiyo,” alisisitiza Kingo.

Aidha Ofisa Elimu Sekondari, Hatujuani Ally alisema Serikali ndiyo inayopanga walimu na hadi sasa imeweza kuleta walimu wa sayansi katika Shule ya Sekondari Nelson Mandela, Matombo, Kibogwa na Mvuha na matarajio ni kuongeza walimu wengi zaidi kwenye shule ambazo zina uhitaji mkubwa.

Ally aliongeza kwamba Wilaya ya Morogoro kwa sasa ina jumla ya walimu wa kufundisha masomo ya sayansi 42 huku mahitaji yakiwa ni walimu 83 katika shule 28 zilizopo.
Share:

Waziri wa Kilimo: Tanzania ina ziada ya Tani 3,013,515 za mazao ya chakula

Kwa mliganisho wa mahitaji na uzalishaji nchi ina ziada ya tani 3,013,515 na imejitosheleza kwa asilimia 123 na 120 mtawalia ambapo uzalishaji katika msimu wa 2016/2017 na 2015/2016 ulikuwa tani 15,900,864 na 16,172,841 mtawalia ambapo mahitaji ya chakula yanayoendana na uzalishaji huo ni tani 13,159,326, na 13,300,034 kwa mwaka wa ulaji 2017/2018 na 2016/2017 mtawalia.

Uzalishaji wa mazao ya chakula katika msimu wa uzalishaji wa 2017/2018 ulifikia tani 16,981,974 zikiwemo tani tani 9,537,857 za mazao ya nafaka na tani 7,354,117 mazao yasiyo nafaka, kiwango ambacho kimeiwezesha nchi kutosheleza mahitaji yake ya chakula ya tani 13,569,285 katika mwaka 2018/2019 kwa kiwango cha utoshelevu (Self Sufficiency Ratio-SSR) cha asilimia 124.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo tarehe 2 Januari 2019 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano maarufu kama Kilimo IV Jijini Dodoma.

Alisema Uzalishaji wa mahindi katika msimu wa 2017/2018, 2016/2017 na 2015/2016 ulikuwa ni tani 6,273,150; 6,680,758 na 6,148,699 mtawalia,wakati mahitaji yanayoendana na uzalishaji huo ni tani 5,462,390; 5,407,499 na 5,202,405 katika miaka ya ulaji ya 2018/2019, 2017/2018 na 2016/2017, Ambapo ziada ya tani 810,760(2018/2019); 1,273,259(2017/2018)  na 946,284(2016/2017) zilipatikana.

Uzalishaji wa mchele katika msimu wa 2017/2018, 2016/2017 na 2015/2016 ulikuwa ni tani 2,219,628; 1,593,609; na 2,229,071 mtawalia,mahitaji yanayoendana na uzalishaji huo ni tani 990,044; 924,435; na 976,925 katika miaka ya ulaji ya 2018/2019, 2017/2018 na 2016/2017,Ziada ya tani 1,229,583(2018/2019); 669,175(2017/2018) na 1,252,146(2016/2017) zilipatikana.

Mhe Hasunga alisema kuwa kutokana na ziada hizo za uzalishaji nchi imeendelea kuwa ghala la chakula kwa nchi jirani. Kwa mfano, kulingana na takwimu za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), katika kipindi cha mwezi Juni 2017 hadi Juni 2018 jumla ya tani 64,477.95 za Mahindi zenye thamani ya shillingi billioni 90.6 na Maharage tani 99,434.45 zenye thamani ya shillingi bilioni 222.0 ziliuzwa katika nchi za DRC, Rwanda, Burundi, Kenya, Uganda, Sudan ya Kusini na Uarabuni.

Hasunga aliongeza kuwa Kati ya mwaka 2015/2016 na 2017/2018 uzalishaji wa mazao ya Asili ya Biashara umeongezeka kwa viwango tofauti tofauti, ambapo zao la korosho kwa sasa linalimwa katika mikoa 17 na Halmashauri 90 hapa nchini baada ya kuanza kwa mpango wa kuongeza uzalishaji wa zao la korosho mnamo mwaka 2013/2014 kupitia uhamasishaji wa kilimo hicho katika mikoa mipya.

Amesema kuwa Mikoa ya asili inayoongoza kwa kilimo cha zao la korosho ni Mtwara, Lindi, Ruvuma, Pwani na Tanga. Katika miaka ya hivi karibuni mikoa mingine mitano nayo imeanza kuzalisha korosho kwa kiasi kidogo ambayo ni Singida, Dodoma, Morogoro, Mbeya na Njombe.

Alisema kuwa taarifa ya uhakiki na malipo kwa wakulima mpaka kufikia tarehe 29 Desemba 2018 tayari Vyama vilivyohakikiwa na kulipwa ni 450.

Malipo yaliyohakikiwa na kuwasilishwa benki ni tsh 231,937,341,674, Malipo yaliyolipwa katika akaunti za Wakulima ni tsh 210,485,753,571, Korosho iliyolipiwa ni Kilo 70,284,043, Kiasi cha Korosho iliyokusanywa katika maghala makuu ni Tani 195,175.844, na Kiasi cha Korosho iliyosombwa na kupelekwa katika maghala ya Hifadhi ni Tani 35,175.844

Katika taarifa yake na waandishi wa habari Mhe Hasunga ameeleza kuwamatumizi ya mbegu bora za pamba yameongezeka kutoka tani 14,500mwaka 2015/2016 hadi tani 18,500 mwaka 2017/2018 na matarajio ni kufikia tani 25,000 msimu wa 2018/2019. Mpaka sasa kiasi cha mbegu tani 27,769 zimesambazwa na ni asilimia 37 zaidi ya kiasi kilichoombwa na Wilayaambacho kilikuwa tani 20,284.

Aidha, Uzalishaji wa chai kavu umeongezeka kutoka tani 32,628 mwaka 2015/2016 hadi kufikia tani 34,010 mwaka 2017/2018. Matumizi ya mfumo wa ushirika umeongeza bei ya kilo moja ya majani mabichi kutoka wastani wa Shilingi 251 mwaka 2015/16 hadi  shilingi 314 mwaka 2017/18. Thamani ya mauzo ya chai nje ya nchi imeongezeka kutoka Dola za kimarekani51,794,854.00 mwaka 2015/2016 hadi kufikia Dola za kimarekani62,167,167.00 mwaka 2017/2018.

Kuhusu zao la Mkonge uzalishaji umeongezeka kutoka tani 39,393 mwaka 2015/16 hadi tani 43,279 mwaka 2017/18. Bei ya tani moja ya Katani daraja la UG mwaka 2015/2016 ilikuwa Shilingi 2,200,000 na mwaka 2017/2018 imefikia Shilingi 3,330,000 sawa na asilimia 50. Thamani ya mauzo ya singa nje ya nchi ni kutoka dola za Kimarekani 35,991,161 mwaka 2015/16 hadi dola za Kimarekani 45,835,845 mwaka 2017/18.

Akieleza kuhusu zao la Sukari Waziri Hasunga amesema kuwa Serikali imeimarisha udhibiti wa uingizaji holela wa sukari kutoka nje hali iliyoimarisha soko la sukari nchini.

Udhibiti huo umechochea ongezeko la uzalishaji wa sukari kutoka tani 293,075 mwaka 2015/2016 hadi takriban tani 307,431.14 mwaka 2017/2018. Aidha, uzalishaji wa sukari unatarajiwa kuongezeka na kufikia tani 352,600 mwaka 2018/2019.

Vilevile, Serikali imeratibu uanzishwaji wa mashamba mapya ya miwa ya Mkulazi I (Ngerengere), Mkulazi II (Mbigiri) na Shamba la Bakhresa –Bagamoyo Sugar (Makurunge).  Sekta ya Sukari kwa ujumla inatoa ajira isiyo ya moja kwa moja kwa watu 57,000 pamoja na kutoa fursa ya ajira kwa watu wengine takriban 75,000 ambao wanahusika na shughuli zinazotoa huduma kwenye mnyororo wa thamani wa uzalishaji wa sukari nchini.
Share:

Waziri wa Nishati autaka Mgodi wa GGM kutumia umeme wa gridi ili walipe kodi stahiki.

WAZIRI Nishati Dk. Medard Kalemani amesema kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa mtambo wa kupoza umeme unaotarajiwa kujengwa Geita, kutawezesha serikali kupeleka umeme wa gridi ya taifa katika Mgodi wa Dhahabu wa Geita (Geita Gold Mine – GGM) na kuondoa sababu ya wao kutokulipa kodi stahiki kwa serikali kwa kigezo cha kutumia mafuta katika uzalishaji.
 
Akikagua eneo utakapojengwa mtambo huo, nje kidogo ya mji wa Geita, Desemba 31 mwaka huu, Waziri Kalemani alisema mtambo huo utafua umeme wa megawati 100 hivyo pamoja na kuwanufaisha wananchi wa Geita na maeneo jirani; utatosheleza pia mahitaji ya mgodi husika ambayo ni takribani megawati 25.
 
“Ni matumaini yangu, kufikia Desemba 2019, GGM watakuwa wameanza kutumia umeme wa gridi ya taifa ili waanze kulipa kodi stahiki kwa serikali. Waache kupata msamaha wa kodi wanaopata sasa kutokana na kuingiza mafuta wanayotumia kuendeshea shughuli zao mgodini,” alisema Waziri.
 
Waziri Kalemani aliongeza kwamba, kuwaunganisha GGM na umeme wa gridi, kutakamilisha azma ya serikali kuwaunganishia umeme wachimbaji wa madini wakubwa wote nchini kwani kwa sasa ni mgodi huo pekee uliobaki.
 
Alimtaka Meneja wa TANESCO Mkoa wa Geita, Mhandisi Joackim Ruweta kuwapa taarifa uongozi wa mgodi huo ili waanze kufanya maandalizi ya kuupokea umeme kwenye miundombinu yao.
 
Akizungumzia kuhusu mradi wenyewe, Waziri Kalemani alieleza kuwa serikali imetoa takribani shilingi bilioni 23 kwa ajili ya kuujenga ili kuboresha hali ya upatikanaji umeme kwa wananchi wa Geita na maeneo jirani.
 
Alisema mradi unahusisha kusafirisha umeme mkubwa kutoka Bulyanhulu, umbali wa kilomita 55 hadi Geita.
 
Aidha, alisema kuwa taratibu zote za maandalizi zimekamilika hivyo akamtaka mkandarasi atakayetekeleza mradi huo, ambayo ni kampuni ya CAMC Engineering kutoka China kuanza mara moja shughuli za ujenzi, ambao kwa mujibu wa mkataba utakamilika ndani ya kipindi cha miezi 17.
 
“Pamoja na kuwa mkataba unabainisha muda wa kukamilisha ujenzi ni miezi 17 lakini tumekubaliana na mkandarasi ajitahidi kukamilisha ndani ya miezi 12,” alifafanua Waziri.
 
Akizungumzia majukumu ya mkandarasi kwa mujibu wa mkataba, Waziri Kalemani alisema yanajumuisha ujenzi wa mtambo wenyewe wa kupoza umeme katika eneo la Mpomvu, nje kidogo ya mji wa Geita, ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Bulyanhulu hadi eneo la mtambo, umbali wa kilomita 55 pamoja na kazi ya kusambaza umeme kwenye vijiji 11 vinavyopitiwa na mradi vikiwemo vya Nyantororo na Buyagu.
 
Waziri aliagiza mambo kadhaa yafanyike katika utekelezaji wa ujenzi wa mradi huo ambayo ni pamoja na kujenga uzio kuzungushia eneo husika kwa sababu za kiusalama pamoja na kuepusha watu kuvamia eneo husika na kujenga makazi.
 
Pia, aliagiza kuanza mara moja kwa kazi za kusafisha eneo husika pamoja na kutoa elimu kwa wananchi ambako mradi unapita ili wajue namna ya kujiandaa kuupokea mradi husika.
 
Waziri Kalemani alikuwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme ambapo mbali na kukagua eneo utakapojengwa mtambo huo, aliwasha umeme Katoro na Buseresere katika vijiji kadhaa pamoja na kuzungumza na wananchi.
Share:

Tamko La Wizara Ya Afya Kulaani Vitendo Vya Ukatili Wa Watoto Majumbani Ikiwemo Mtoto Kufungiwa Kabatini

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inalaani na kukemea vikali vitendo vya ukatili dhidi ya watoto vinavyoendelea kujitokeza nchini. Vitendo hivi vinafanywa na kuhusisha ndugu na walezi wa karibu wa wataoto hivyo kuzua hofu kubwa kwa watoto na jamii kwani vinaathiri malezi na makuzi ya awali ya watoto kwa kutozingatia haki zao za msingi.

Mapema wiki hii, imeripotiwa  mwalimu wa shule ya msingi jijini Dodoma  (jina limehifadhiwa) ambaye anatuhumiwa kumfungia mtoto mdogo ndani ya kabati kwa kipindi kirefu na kusababisha afya ya mtoto huyo kudhohofika. Mwalimu huyo anatuhumiwa pia kumfanyia vitendo vya ukatili mama mzazi wa mtoto  huyo kwa kumpiga na kumsababishia maumivu mwilini yaliyopelekea binti huyo na mtoto wake kulazwa.

Kipekee, Wizara inawapongeza wanajamii wote walioibua tukio hili na kuwezesha Jeshi la Polisi kumkamata mtuhumiwa kwa ajili ya uchunguzi ili Sheria iweze kuchukua mkondo wake. TunaaminiJeshi la Polisi watafanya upelelezi wa tukio hili kwa weledi mkubwa ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa.

Matukio ya ukatili wa watoto yanapotokea majumbani yanarudisha nyuma jitihada za Serikali za kulinda na kuendeleza haki na ustawi wa watoto katika ngazi ya familia ambayo ndio kitovu cha jamii wakiwemo na watoto.

Kufuatia kitendo hicho kilichofanywa na mwalimu wa shule ya msingi ambaye ni mlezi wa watoto, Wizara inawataka wazazi, walezi na jamii kuzingatia wajibu wa ulinzi wa watoto ili kuwahakikishia usalama wao katika maeneo ya majumbani, shuleni, mtaani, njiani na katika jamii kwa ajili ya kutekeleza lengo la kupunguza matukio ya ukatili kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2021/2022.

Aidha, Wizara inatoa rai kwa jamii na wananchi wema kuwa makini na matumizi ya mitandao ya kijamii ili kuepuka makosa ya kisheria yanayoweza kutokea kwa kusambaza, kuchapisha na kupiga picha za watoto ambao ni wahanga wa ukatili na kuziweka wazi kinyume na Sheria ya Mtoto Na. 21 ya Mwaka 2009.

Wizara inatoa pole kwa wazazi, ndugu, marafiki na familia ya mtoto aliyefanyiwa ukatili huo. Tunawaomba wanajamii kuendelea kutoa ushirikiano katika kufichua vitendo vyote vya ukatili dhidi ya watoto vinavyojitokeza katika maeneo yao. Aidha, katika kipindi hiki ambapo uchunguzi unaendelea kufanyika tunaomba pawe na utulivu na uvumilivu ili kutoa nafasi kwa vyombo vya dola kufanya uchunguzi kwa makini na Sheria iweze kuchukua mkondo wake.

Imetolewa na
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto
(Idara Kuu Maendeleo ya Jamii)
02/01/2019
Share:

Naibu Waziri Shonza Awataka Wasanii Kujijengea Tabia Ya Kujiwekea Akiba

Naibu waziri wa Habarui, sanaa utamaduni na michezo Mhe. Juliana Shonza amewataka wasanii wa Injili kjijengea tabia ya kujiwekea akiba ili punde wapatapo matatizo waweze kuyatatua kwa urahisi.

Ameyasema hayo hivi karibuni alipokuwa akizindua mfuko wa Tagoane LoanFund Jijini Arusha ambapo amepongeza uongozi wa Tagoane kufikia hatua hiyo. Ameyataka mashirikisho yote ya muziki wa Injili nchini Tanzania kuiga mfano nzuri wa Tagoane ili waweze kuwa na mashirikisho ambayo ni hai na yanayoleta mshindo kwenye jamii.

Amesema yeye kama mlezi wa wasanii wote nchi amewaomba waamke wachangamkie fursa na wasiwe wavivu kujifunza kutoka kwa wenzao waliofanikiwa .Amewataka wasanii kukaa kwa pamoja Kuonyeshe Uzalendo kwa nchi yao wajadili changamoto mbalimbali wanazozipitia na kutafuta namna ya kutazua changamoto zinazowakabili.

Kwa upande wake Rais wa Tagoane Taifa Dkt. Godwin Maimu amesema kuwa wanedhamiria kuanzisha mfuko wao wa Tagoane Loan Fund ambapo mpaka sasa umekuwa na wanachama ambao wameshachangia akiba zao zipatazo shilingi milioni kumi.Amesema mfuko huo unatarajiwa kuanza kutoa mikopo kwa wanachama wavhqngiaji kuanzia 2 januari 2019

Maendeleo kama vijana hayawezi kuendelea ukiwa na jitihada za mtu mmoja mmoja bali balintunapounganisha nguvu zetu kwa pamoja mwisho wa siku tunapata kitu cha kuweza kutusaidia. Alisema Dkt Maimu

Amesema lengo la mfuko huo ni kuwakwamua wasanii watakaokuwa na miradi ya uwekezaji, makampuni makubwa, na watakaoweza kutoa fursa na ajira kwa vijana hapa nchini na kulipa kodi kama wananchi wengine

Aidha tamasha hilo lililoshorikisha wasanii mbalimbali wakiwemo wajasiriamali, wachoraji, wachongaji, sanaa za ubunifu ni fursa ambayo Tagoane wameileta na kuwataka wasanii waitumie kwaajili ya kujikwamua kiuchumi na kuoata maendeleo katia jamii nzima

Tamasha hilo la Tukuza festival lilizinduliwa rasmi mwaka 2017 likiwa linafanyika kwa mara ya pili limebeba kauli mbiu isemayo toto yatima haihitaji chakula a mavazi peke yake ila awezeshwe nyenzo za kutimiza malengo yake.
Share:

IDADI YA WASOMAJI

TUSIKILIZE LIVE KUPITIA TUNEIN

UNGANA NASI FACEBOOK HAPA

10 ZILIZOSOMWA ZAIDI

Labels