Sports


MACHI 1, 2012
STARS, MAMBAS ZAINGIZA MIL 64/-
Mechi ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika- AFCON 2013 kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Msumbiji (Mambas) iliyochezwa jana (Februari 29 mwaka huu) imeingiza sh. 64,714,000.

Ofisa Habari Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), BONIFACE WAMBURA amesema fedha hizo zimepatikana kutokana na watazamaji 16,776 waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo lililochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Sehemu iliyoingiza watazamaji wengi ilikuwa viti vya bluu na kijani ambapo 14,403 walikata tiketi kwa kiingilio cha sh. 3,000 kwa kila mmoja. Viingilio vingine katika mechi hiyo vilikuwa sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 10,000 kwa VIP C, sh. 15,000 viti vya VIP B wakati VIP A iliyoingiza watazamaji 91 kiingilio kilikuwa sh. 20,000.

Mgawanyo wa mapato hayo ni kama ifuatavyo; asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ilikuwa sh. 9,871,627, gharama ya kuchapa tiketi sh. 4,500,000, malipo kwa waamuzi wane na kamishna wa mchezo huo sh. 12,180,000 na ulinzi na usafi kwa Uwanja wa Taifa sh. 2,350,000.

Malipo kwa Wachina (Beijing Construction) sh. 2,000,000, maandalizi ya uwanja (pitch marking) sh. 400,000 wakati asilimia 20 ya gharama za mchezo ni sh. 6,682,475.

Mgawo mwingine ni asilimia 10 ya uwanja sh. 3,341,237, asilimia 5 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 1,670,136 na asilimia 65 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh. 21,718,042.



FEBRUARI, 29, 2012
LINE UP ya Taifa Stars katika mechi ya leo dhidi ya Msumbiji inayochezwa jijini Dar es Salaam katika uwanja wa taifa:

Juma Kaseja 1
Shadrack Nsajigwa 14
Stephen Mwasika 3
Juma Nyoso 4
Aggrey Morris 6
Shabani Nditi 19
Nizar Khalfan 16
Mwinyi Kazimoto 15
John Bocco 9 
Abdi Kassim 13
Vincent Barnabas 17 

Substitutes:
Mwadini Ally 18
Shomari Kapombe 20
Waziri Salum 21
Salum Abubakar 11
Mrisho Ngassa 8
Hussein Javu 12
Nsa Job 10



KITUO CHA TELEVISHENI CHA KLABU YA SIMBA(simba tv) KUZINDULIWA RASMI  KESHO KUTWA IJUMAA
KLABU ya soka ya Simba inatarajiwa kuzindua Simba Tv siku ya Ijumaa katika hoteli ya JB Belmont iliyopo katika jengo la Benjamin Mkapa, katikati ya jiji la Dar es Salaam.
Leo jijini Dar es Salaam msemaji wa Simba EZECKIEL KAMWAGA amesema, Simba Tv itakuwa ikirushwa katika kituo cha Televisheni cha Clouds Fm ambapo itakuwa ikizungumzia masuala mbalimbali yahusuyo klabu hiyo.
Amesema uzinduzi huo utakaokuwa kwa wageni waalikwa tu huku kwa wengine watakaotaka kuhudhuria watapaswa kulipa shilingi 70,000 kwa kila mtu, utaambatana na burudani mbalimbali sambamba kuonyeshwa historia ya Simba.
xxxxxxxxxxxxxxxxx
Katika juhudi za kuwaenzi wanamichezo walioliletea sifa kubwa taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Nchini (TPBC) iko kwenye mchakato wa kuanzisha Taasisi ya Michezo ya Rashid Matumla (Rashid Matumla Sports Academy) ya kuibua vipaji vya vijana wanaochipukia katika michezo hususan ngumi.


Huu ni mkakati wa kumwandaa bingwa wa zamani wa dunia aliyetambuliwa na Umoja wa Ngumi wa Dunia (Rashid Matumla) kustaafu ngumi ili aweze kutumia kipaji chake cha ngumi kuendeleza vijana. 



TPBC inajivunia historia nzuri ya Rashid Matumla kwa kuwa bondia wa kwanza Tanzania kuwa bingwa wa dunia aliyetambuliwa na Umoja wa Ngumi wa Dunia (WBU) pamoja na sifa kemkem alizoliletea taifa hili kipindi hiki chote anachopigana ngumi. Tunapenda kuutangazia umma kuwa tunamwandalia Rashid Matumla mazingira mazuri ya kustaafu ngumi.


Katika taasisi hiyo ya Rashid Matumla Sports Academy, Rashid atakuwa ndiye Rais na atakuwa analipwa mshahara kama mwajiriwa kwa kipindi chote cha uhai wa taasisi hiyo na kumfanya aweze kujipatia ajira ya kudumu wakati hachezi tena ngumi. Huu ni moja ya mikakati ya TPBC kuhakikisha kuwa mabondia wake walioiletea nchi hii heshima kubwa wanaenziwa kwa kuandaliwa maisha mazuri wanapostaafu ngumi!


Ni lazima kama taifa tuwajali wale wote wanaolipigania taifa hili na tutaendelea pia kuandaa mazingira mengine ya kuwawezesha waishi vizuri na kuheshimiwa daina ili kuleta changamoto kwa wengine ili nao wapigane kufa na kupona kuliletea sifa taifa letu katika michezo.


Taasisi hii itazinduliwa rasmi wakati wa mpambano wa Rashid Matumla na Vitaly Shemetov bondia anayetoka Urusi litakalofanyika mjini Moshi tarehe 22nd Juni na kuhudhuriwa na Mcheza sinema maarufu wa Marekani, Deidre Lorenz wa sinema maarufu ya Santorini Blue. Mcheza sinema huyo atakuwepo nchini kwa ajili ya kukimbia mbio zaMarie Frances Mt. Kilimanjaro Marathon kusheherekea miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika zikazofanyika tarehe 24 Juni mwaka huu kuanzia Moshi Club.


Taasisi ya Rashid Matumla Sports Academy ambayo itakuwa inafanya kazi nchi nzima itajumuisha pia bingwa mwingine wa zamani wa dunia aliyetambuliwa na Umoja wa Ngumi wa Dunia (WBU) Magoma Shaban. Hawa wote watakuwa waajiriwa wa taasisi ya Rashid Matumla Sports Academy wakifanya kazi za kuibua vipaji kwa vijana Tanzania nzima!


Wakati huo huo: Kemisheni ya Ngumi za Kulipwa Nchini (TPBC) imetoa kibali cha mapambano sita (6) ya ubingwa wa taifa yatakayofanyika jijini Tanga tarehe 4/3/2012 siku ya jumapili.



Ubingwa wa Taifa:


1. J.J. Ngotiko Vs. Ibrahim Habibu Bantamweight  (10 rounds)
2. Jumanne Mohammed Vs. na Juma Mokiwa Featherweight.(10 rounds)
3. Haji Juma Vs. Omari saidi Flyweight weight (10 rounds)
4. Athumani Boxer Vs. Lucas Michael Lightweight ( 10 rounds)
5. Saidi Mundi Vs. Saimon Zablon Super Featherweight ( 10 rounds)
6. Zeberi Kitandula Vs. Bakari Shendeka (Super bantam) ( 10 rounds)


Mapambano ya utangulizi yasiyo ya ubingwa.


1. Alibaba Ramadhani Vs. Juma Kihio Light Middleweight  (8 rounds)
2. Hassan Ngonyani Vs. Puguto Omari Super Flyweight  6 rounds)
3. Patric Kimweri Vs. Issa Omari (light flyweight  6 rounds)
          




FEBRUARI 24, 2012
KOZI YA MADAKTARI WA TIBA YA MICHEZO
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeandaa kozi ya awali ya madaktari au wataalamu wa viungo (physiotherapist) kwa klabu za Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza itakayofanyika jijini Dar es Salaam.

Kozi hiyo ya siku tano itakayoanza Machi 5-9 mwaka huu itakuwa na washiriki 32 tu. Kila klabu inatakiwa kutuma mshiriki mmoja ambapo anatakiwa kuwa daktari wa timu au physiotherapist.

Katika sifa za kitabibu, washiriki wanatakiwa wawe Clinical Officer (Medical Assistant), Assistant Medical Officer na Medical Officer au Physiotherapist. Ada ya kushiriki ni sh. 60,000.

Washiriki wanatakiwa kutuma TFF wasifu wao (CV) na nakala za vyeti vyao vya kitaaluma na mwisho wa kuthibitisha kushiriki kozi hiyo ni Machi Mosi mwaka huu. Kwa madaktari wanatakiwa wawe ambao kwa sasa wanazitumia klabu husika (active).

Kila klabu itamgharamia mshiriki wake kwa malazi, nauli ya kuja na kurudi pamoja na posho wakati TFF itatoa vifaa vya kozi (stationeries), chai na chakula cha mchana.

VIINGILIO STARS VS MSUMBIJI
Kiingilio cha chini katika mechi ya mchujo ya Kombe la Mataifa ya Afrika kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Msumbiji (Mambas) itakayochezwa Februari 29 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni sh. 3,000.

Jumla viti 36,693 (rangi ya bluu na kijani) ndivyo vitakavyotumika kwa kiingilio hicho katika uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 60,000 wakiwa wameketi.  

Viingilio vingine ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 10,000 kwa VIP C, sh. 15,000 kwa VIP B wakati kwa watakaokuwa miongoni mwa watakaokaa katika viti VIP A ambavyo viko 748 tu watalazimika kulipa sh. 20,000 kwa kila mmoja.

Tiketi zitaanza kuuzwa siku moja kabla ya mchezo katika vituo vya Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Kituo cha mafuta cha Bigbon kilichopo Msimbazi (Kariakoo), mgahawa wa Steers ulioko Barabara ya Samora/Ohio, Kituo cha mafuta cha Oilcom Ubungo na Uwanja wa Taifa.

MWENYEJI KITUO CHA FAINALI FDL
Mkoa unaotaka kuwa mwenyeji wa fainali za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) zinazoshirikisha timu tisa bora za ligi hiyo unatakiwa kutoa sh. milioni 25 ambazo ni gharama za kuendesha fainali hizo.

Haki ya kuwa mwenyeji wa fainali hizo iko wazi kwa mikoa yote wanachama wa TFF ingawa tayari ipo minne ambayo imeshatuma rasmi maombi ya kuandaa fainali hizo. Mikoa hiyo ni Mbeya, Mwanza, Ruvuma na Tabora.

Kwa mikoa ambayo itakuwa tayari kuwa mwenyeji kwa maana ya kutimiza sharti hilo la kutoa kiasi hicho cha fedha inatakiwa iwe imefanya hivyo kufikia Machi 15 mwaka huu.

Pia kumefanyika mabadiliko ya kuanza fainali hizo, sasa zitaanza Machi 31 mwaka huu badala ya Machi 17 ambayo ilitangazwa awali.

MAPATO STARS VS DR CONGO
Pambano la kirafiki la kimataifa kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-DRC (Leopards) lililofanyika jana (Februari 23 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam limeingiza sh. 32,229,000.

Fedha hizo zimepatikana kutokana na watazamaji 11,420 waliokata tiketi kushuhudia mechi kwa kiingilio cha sh. 2,000, sh. 5,000, sh. 7,000, sh. 10,000 na sh. 15,000.

Mgawanyo wa mapato hayo ulikuwa kama ifuatavyo; asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ni sh. 5,916,288, gharama ya kuchapa tiketi sh. 2,250,000, malipo kwa kamishna wa mchezo sh. 150,000, malipo kwa waamuzi wanne sh. 480,000, ulinzi na usafi kwa Uwanja wa Taifa sh. 2,350,000, Wachina sh. 2,000,000, umeme sh. 300,000 na maandalizi ya uwanja (pitch marking) sh. 400,000.

Nyingine ni asilimia 20 ya gharama za mchezo sh. 3,676,542, asilimia 10 ya uwanja sh. 1,838,271, asilimia 5 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 919,136 na asilimia 65 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh. 11,948,763.


FEBRUARI21, 2012
Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ilikutana Februari 15 mwaka huu jijini Dar es Salaam na kufanya uamuzi kwa ajenda mbalimbali ikiwemo Marekebisho ya Katiba za Wanachama wa TFF, na pia ushauri wa kisheria ulioombwa kwake na Kamati ya Uchaguzi ya TFF.

Uamuzi uliofanywa kwa wanachama wote 40 wa TFF ni ufuatao; wanachama wote wanatakiwa kufanya marekebisho kwenye katiba zao katika maeneo matatu kwa mujibu wa maelekezo ambayo TFF ilitoa mwaka jana.

Maeneo hayo ni sifa za wagombea uongozi ambapo kwenye kipengele cha elimu ni lazima iwe kuanzia kidato cha nne, kutopeleka masuala ya mpira wa miguu katika mahakama za kawaida na kamati zao za uchaguzi kufanya kazi chini ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF.

Hivyo hakuna mwanachama yeyote wa TFF anayeruhusiwa kufanya uchaguzi kwa sasa kama katiba yake ina upungufu au inakwenda kinyume na maelekezo kuhusu maeneo hayo matatu.

Kamati imetoa hadi Juni Mosi mwaka huu kwa wanachama ambao katiba zao zina upungufu katika maeneo hayo wawe wamefanya marekebisho ndiyo waendelee na uchaguzi kwa wale ambao muda wa uchaguzi umefika.

Ushauri wa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji kwa Kamati ya Uchaguzi ya TFF ni kuwa katiba zote za wanachama ziwe na vitu hivyo vitatu.




SIKU YA WANAWAKE DUNIANI- MACHI 8
Machi 8 kila mwaka ni Siku ya Wanawake Dunia. Ili kuadhimisha siku hiyo kwa upande wa mpira wa miguu, TFF kwa kushirikiana na Chama cha Mpira wa Miguu cha Wanawake (TWFA) imeandaa mashindano mafupi kwa shule nane za sekondari za Mkoa wa Dar es Salaam.

Mashindano yataanza Februari 24 mwaka huu kwenye viwanja viwili vya Jitegemee Sekondari ambapo kutakuwa na kundi B wakati kundi A litacheza mechi zake Makongo Sekondari. Mechi zitaanza saa 8 mchana na kumalizika saa 10 jioni.

Kundi A lina shule za Makongo, Goba, Twiga na Lord Barden wakati Jitegemee, Benjamin Mkapa, Kibasila na Tiravi zitakuwa kundi B.

Lengo la mashindano ni kuhamasisha mpira wa miguu kwa wasichana katika ngazi ya shule, kuandaa, kubaini na kuendeleza mafanikio yanayopatikana katika timu ya wanawake ya Taifa.

Pia kutoa fursa kwa watoto wa kike kusherehekea Siku ya Wanawake duniani kupitia mpira wa miguu, kutekeleza ushiriki wa TFF katika shughuli za kijamii na ni sehemu ya mchakato wa kuandaa mashindano ya ligi kwa wasichana.

Uchaguzi wa timu shiriki umezingatia mchango wa shule katika kuendeleza mpira wa miguu kwa wasichana/wanawake. Pia zawadi zitatolewa kwa mshindi wa kwanza, pili na tatu.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mashindano hayo ni Zainab Mbiro kutoka Twiga Sekondari wakati wajumbe ni Brighton Mbasha                (Jitegemee), Yusuf Mohamed (Tiravi), Michael Bundala (TFF), Furaha Francis (TFF/TWFA) na Rose Kissiwa (TWFA).

Tunaomba wadau mbalimbali wajitokeze kusaidia gharama za uendeshaji wa mashindano hayo. 

FAINALI FDL KUANZA MACHI 17
Hatua ya fainali ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) itafanyika kuanzia Machi 17 mwaka huu katika kituo ambacho kitatangazwa baadaye.

Timu tatu kutoka katika kila kundi ndizo zitakazocheza fainali hiyo. Washindi watatu wa juu ndiyo watakaofuzu kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao.

Mikoa mitatu ya Mbeya, Mwanza na Ruvuma imewasilisha maombi ya kuwa wenyeji wa fainali hizo. Maombi hayo yanafanyiwa uchambuzi kabla ya kutangaza mkoa uliopewa nafasi hiyo.

Wakati huo huo, michuano ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) hatua ya makundi inamalizika kesho (Februari 22 mwaka huu) kwa mechi tatu za kundi A.

Polisi Dar es Salaam watakuwa wenyeji wa Morani FC ya mkoani Manyara katika mechi itakayochezwa Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani.

Mgambo Shooting Stars ya Tanga itaoneshana kazi na Temeke United ya Dar es Salaam katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga wakati Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro utashuhudia mechi kati ya wenyeji Burkina Faso na Transit Camp ya Dar es Salaam.




FEBRUARI, 19, 2012

*KOCHA DRC AWASILI, TIMU KUTUA JUMANNE

*TAIFA STARS KUINGIA KAMBINI KESHO, TAYARI KUIKABILI DRC NA MSUMBIJI

KOCHA mkuu wa timu ya Taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), CLAUDE LE ROY na msaidizi wake wamewasili nchini jana mchana (Februari 18 mwaka huu) kwa ndege ya Emirates wakitokea Paris, Ufaransa tayari kwa mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Taifa Stars.

Mechi hiyo itafanyika Februari 23 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa,  jijini Dar es Salaam.

Mfaransa Le Roy ambaye alianza kuifundisha DRC mwezi Septemba mwaka jana na msaidizi wake wamefikia kwenye hoteli ya Golden Tulip.

Ofisa Habari wa shirikisho la mpira wa miguu  nchini  (TFF), Boniface Wambura amesema msafara mzima wa timu hiyo wenye watu 24 wakiwamo wachezaji 19 utawasili nchini Jumanne (Februari 21 mwaka huu) na kufikia kwenye hoteli ya Holiday Inn.

Februari 22 mwaka huu (saa 5 asubuhi) kutakuwa na mkutano wa makocha wa timu zote Jan Poulsen (Taifa Stars) na Le Roy (DRC) utakaofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Wakati huo huo, kikosi cha Taifa Stars kilichotangazwa Februari 16 mwaka huu na Kocha Poulsen kesho (Februari 20 mwaka huu) kinaingia kambini jijini Dar es Salaam tayari kwa mechi dhidi ya DRC na ile ya michuano ya AFCON 2013 dhidi ya Msumbiji ambayo itachezwa Februari 29 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa.

FEBRUARI 17, 2012

MAREKEBISHO RATIBA VPL
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limefanya marekebisho madogo kwenye ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kupisha mechi mbili za Taifa Stars zinazotarajiwa kuchezwa Februari 23 na 29 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Taifa Stars itacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) ambayo itafanyika Februari 23 mwaka huu wakati ile ya mashindano dhidi ya Msumbiji itachezwa Februari 29 mwaka huu.

Marekebisho hayo yamefanywa kutokana na makubaliano yaliyofikiwa na klabu za Ligi Kuu ya Vodacom kuwa pale ambapo Taifa Stars itakuwa na mechi, ligi itasimama kupisha mechi husika.

Tarehe mpya za mechi husika na namba zake ni kama ifuatavyo; mechi namba 131 kati ya JKT Ruvu na Toto Africans sasa itachezwa Machi 3 mwaka huu, mechi namba 132 kati ya Yanga na Azam (Machi 10 mwaka huu), mechi namba 133 kati ya JKT Oljoro na Kagera Sugar (Machi 3 mwaka huu).

Mechi namba 134 kati ya Polisi Dodoma na Kagera Sugar (Machi 11 mwaka huu), mechi namba 135 kati ya Moro United na JKT Ruvu (Machi 3 mwaka huu), mechi namba 136 kati ya African Lyon na Ruvu Shooting (Machi 7 mwaka huu) na mechi namba 137 kati ya JKT Oljoro na Toto Africans (Machi 7 mwaka huu).

Timu zilizotajwa mwanzo ndizo zitakazokuwa zinacheza kwenye viwanja vyake vya nyumbani.

MECHI ZA VPL WIKIENDI HII
Wikiendi hii kutakuwa na mechi nne za VPL. Mechi za Jumapili (Februari 19 mwaka huu) ni kati ya Coastal Union itakayoikaribisha Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga wakati Villa Squad itakuwa mgeni wa Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro. Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Polisi Dodoma.

LIGI DARAJA LA KWANZA (FDL)
Mechi za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) zinaendelea wikiendi hii ambapo kesho (Februari 18 mwaka huu) kutakuwa na mechi ya Kundi C kati ya Polisi Morogoro na Rhino FC ya Tabora itakayochezwa Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Keshokutwa (Februari 19 mwaka huu) Kundi A ni kati ya Morani FC na Temeke United zitacheza mkoani Manyara na Februari 20 mwaka huu ni Transit Camp na Polisi Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Burkina Faso na Mgambo Shooting kwenye Uwanja wa Jamhuri.

Kundi B Februari 19 mwaka huu Small Kids itaikaribisha Mbeya City kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, Mlale na Polisi Iringa kwenye Uwanja wa Majimaji na Tanzania Prisons na Majimaji kwenye Uwanja wa Sokoine.



FEBRUARI 16, 2012
POULSEN ATAJA 23 KUIVAA MSUMBIJI
Kocha wa timu ya Taifa (Taifa Stars), Jan Poulsen leo (Februari 16 mwaka huu) ametangaza kikosi cha wachezaji 23 kwa ajili ya mechi ya mchujo ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) ambalo fainali zake zitafanyika mwakani nchini Afrika Kusini.

Kabla ya kuivaa Msumbiji kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mechi itakayochezwa Februari 29 mwaka huu, kikosi hicho kinatarajia kucheza mechi ya kirafiki Februari 23 mwaka huu dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) itakayofanyika kwenye uwanja huo huo.

Wachezaji wapya walioitwa kwa mara ya kwanza kwenye kikosi hicho kitakachoingia kambini Februari 20 mwaka huu jijini Dar es Salaam ni viungo Jonas Gerald (Simba) na Salum Abubakar (Azam).

Kikosi kamili kinaundwa na makipa Shabani Kado (Yanga), Juma Kaseja (Simba) na Mwadini Ali (Azam). Mabeki ni nahodha Shadrack Nsajigwa (Yanga), Masoud Cholo (Simba), Aggrey Morris (Azam), Juma Nyoso (Simba), Juma Jabu (Simba), Stephen Mwasika (Yanga) na Kelvin Yondani (Simba).

Viungo ni Jonas Gerard (Simba), Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), Shomari Kapombe (Simba), Salum Abubakar (Azam), Mwinyi Kazimoto (Simba) na Abdi Kassim (Azam).

Washambuliaji ni Hussein Javu (Mtibwa Sugar), John Bocco (Azam), Nizar Khalfan (Philadelphia Union, Marekani), Mrisho Ngasa (Azam), Ally Badru Ally (Canal Suez, Misri), Uhuru Selemani (Simba) na Nsa Job (Villa Squad).

AFC NAYO YASHUKA DARAJA
Timu ya AFC ya Arusha imeshindwa kutokea kwenye mechi ya Kundi C ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) dhidi ya 94 KJ iliyokuwa ichezwe jana (Februari 15 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani.

Kwa mujibu wa Kanuni ya 21 ya FDL timu yoyote inayoshindwa kufika kituoni na kusababisha mchezo husika kutochezwa itashushwa daraja hadi Ligi ya Taifa na matokeo ya michezo yake yote itafutwa ili kutoa uwiano sahihi kwa timu zilizobaki kwenye mashindano.

Si Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), msimamizi wa ligi hiyo Kituo cha Pwani wala Kamishna wa mechi hiyo Ramadhan Mahano waliokuwa na taarifa yoyote ya mapema juu ya AFC kushindwa kufika kituoni.

AFC ambayo mbali ya kushushwa daraja inatakiwa kulipa faini ya sh. milioni moja kabla ya kucheza Ligi ya Taifa msimu ujao. Sh. 500,000 kati ya hizo zitakwenda kwa timu ya 94 KJ iliyoingia gharama za kujiandaa kwa mechi hiyo ambapo wapinzani wao hawakufika uwanjani.

Kundi C la ligi hiyo sasa linabakiwa na timu nne baada ya Manyoni FC ya Singida nayo kushuka daraja kwa kushindwa kucheza mechi yake dhidi ya Polisi Tabora iliyokuwa ifanyike Februari 12 mwaka huu Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.

Timu zilizobaki katika kundi hilo ambalo baada ya mbili kujitoa hakuna itakayoshuka daraja ni 94 KJ ya Dar es Salaam, Polisi Tabora, Polisi Morogoro na Rhino FC ya Tabora.



FEBRUARI 14, 2012
LIGI kuu ya Vodacom inaingia raundi ya 18 kesho (Februari 15 mwaka huu) kwa mechi nne zitakazochezwa viwanja vya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha, Azam Chamazi jijini Dar es Salaam, Mkwakwani jijini Tanga na Kaitaba mjini Bukoba.

Mwamuzi ISRAEL MUJUNI atazichezesha JKT Oljoro na Ruvu Shooting jijini Arusha, Azam na Villa Squad zitachezeshwa na JUDITH GAMBA jijini Dar es Salaam, ODEN MBAGA ndiye atapuliza filimbi kwenye mechi ya Coastal Union na JKT Ruvu jijini Tanga.

Mjini Bukoba kutakuwa na mechi kati ya Kagera Sugar na Moro United.

Mechi nyingine ya raundi ya 18 itachezwa keshokutwa (Februari 16 mwaka huu) kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza ambapo Toto Africans itakuwa mwenyeji wa Mtibwa Sugar.

XXXXXXXXXXXXXXX
TIMU ya Manyoni FC ya Singida imeshindwa kutokea kwenye mechi ya Kundi C ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) dhidi ya Polisi Tabora iliyokuwa ichezwe juzi (Februari 12 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.

Ofisa Habari Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Boniface Wambura amesema  kwa mujibu wa Kanuni ya 21 ya ligi hiyo timu yoyote inayoshindwa kufika kituoni na kusababisha mchezo husika kutochezwa itashushwa daraja hadi Ligi ya Taifa na matokeo ya michezo yake yote itafutwa ili kutoa uwiano sahihi kwa timu zilizobaki kwenye mashindano.

Amesema si TFF, msimamizi wa ligi hiyo Kituo cha Tabora, Alfred Sitta wala Kamishna wa mechi hiyo Charles Komba waliokuwa na taarifa yoyote ya mapema juu ya Manyoni FC kushindwa kufika kituoni.

Manyoni FC ambayo mbali ya kushushwa daraja inatakiwa kulipa faini ya sh. milioni moja kabla ya kucheza Ligi ya Taifa msimu ujao.
Timu hiyo  ilikuwa Kundi C pamoja na timu za 94 KJ ya Dar es Salaam, AFC ya Arusha, Polisi Tabora, Polisi Morogoro na Rhino FC ya Tabora.



XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
TIMU nane zinaingia viwanjani kesho (Februari 15 mwaka huu) kusaka pointi tatu katika mechi za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ambayo sasa iko katika mzunguko wa pili hatua ya makundi.

Kundi B ni kati ya Majimaji na Small Kids zitakazooneshana kazi Uwanja wa Majimaji mjini Songea wakati Mbeya City itaumana na Polisi Iringa kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.

Mechi za Kundi C zitakuwa kati ya Polisi Morogoro na Polisi Tabora kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro huku 94 KJ ikiwa mwenyeji wa AFC katika Uwanja wa Mabatini mjini Mlandizi.

Keshokutwa (Februari 16 mwaka huu) Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga utakuwa mwenyeji wa mechi ya Kundi A kati ya Mgambo Shooting na Polisi Dar es Salaam jijini Tanga. Februari 17 mwaka huu kwenye uwanja huo huo kutakuwa na mechi kati ya Transit Camp na Morani ya mkoani Manyara.

Mechi nyingine ya Kundi B itapigwa keshokutwa (Februari 16 mwaka huu) ikizikutanisha timu za Tanzania Prisons na JKT Mlale kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.



FEBRUARI 13, 2012


MASHINDANO ya ligi ya taifa ngazi ya mkoa  wa shinyanga msimu wa mwaka  2011/2012 katika hatua ya kwanza inatarajia kuanza kutimua vumbi  februari 15 mwaka huu katika vituo   vinne vya wilaya ya Bariadi, Maswa, manispaa ya Shinyanga  na kahama

Akizungumza na dawati la michezo la kahama fm katibu mkuu wa chama cha soka mkoani shinyanga [SHIREFA] IBRAHIM MAGOMA  amesema timu zote zinazoshiriki ligi hiyo zinatakiwa kufuata ipasavyo kanuni  za mashindano pamoja na utaratibu uliopangwa kama walivyoandikiwa katika barua za kushiriki ligi hiyo ikiwamo kukamilisha  malipo wanayodaiwa.

Pia amewataka  viongozi wa timu  kufika  katika kikao cha maandalizi ya mchezo  asubuhi wakiwa na vifaa vyote vitakavyotumika katika mchezo.

Wanaotakiwa kufika ni kocha, mtunza vifaa, nahodha, daktari na  mchua misuli wa wachezaji

Katika hatua hiyo ya kwanza kila  kundi litatoa washindi  wawili watakaoingia hatua ya pili  itakayoshirikisha jumla ya timu nane

Xxxxxxxxxxxxxxxx
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha aliyewahi kuwa mjumbe wake wa Kamati ya Utendaji, Kassim Kashulwe kilichotokea Februari 9 mwaka huu nyumbani kwake Kigurunyembe mkoani Morogoro.

Licha ya kuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF (wakati huo Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania- FAT), pia Kashulwe aliwahi kuwa kiongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Morogoro (MRFA) na baadaye kamishna wa mechi za Ligi Kuu.

Ofisa Habari  WA TFF, Boniface Wambura amesema amesema chama cha soko Morogoro (MRFA) kimewataarifu kuwa, Kashulwe alifia nyumbani kwake na kuzikwa juzi (Februari 11 mwaka huu) kwenye makaburi ya Kora yaliyoko nje kidogo ya mji wa Morogoro.

Mbali ya Kashulwe, wengine waliochaguliwa katika uchaguzi wa FAT uliofanyika mwaka 1993 mjini Kibaha ni Muhidin Ndolanga (Mwenyekiti), Alhaji Omari Juma (Makamu Mwenyekiti) na Kanali Ali Hassan Mwanakatwe (Katibu Mkuu) na wajumbe Abdul Msimbazi, Amin Bakhresa, Job Asunga, Joel Bendera, Masalu Ngofilo na Wilson Mwanja.

Msiba huo ni pigo kwa familia ya Kashulwe, TFF na familia ya mpira wa miguu nchini kwa kuwa mchango wake ulikuwa bado unahitajika.

TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Kashulwe, na MRFA na kuwataka kuwa na uvumilivu kipindi hiki cha msiba huo mzito. Pia TFF itatoa ubani wa sh. 200,000 kwa familia ya marehemu kama rambirambi zake.

Mungu aiweke roho ya marehemu Kashulwe mahali pema peponi. Amina


xxxxxxxxxxxxxxxx
WATAZAMAJI 14,150 ndiyo waliokata tiketi kushuhudia pambano la Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Yanga na Ruvu Shooting lililochezwa jana (Februari 12 mwaka huu) katika uwanja wa taifa, jijini  Dar es Salaam na kuingiza sh. 47,554,000.

Hata hivyo Ofisa Habari Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Boniface Wambura amesema ni watazamaji saba tu waliokata tiketi za VIP A zilizokuwa zikiuzwa sh. 15,000. Viingilio vingine vilikuwa sh. 10,000 kwa VIP B na C, sh. 5,000 viti vya rangi ya chungwa na kiiingilio cha sh. 3,000 kwa viti vya bluu na kijani kilichovutia watazamaji 12,853.

Baada ya kuondoa gharama za awali za mechi hiyo namba 119 na asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni sh. 7,254,000 kila timu ilipata sh. 8,583,000 wakati mgawo wa uwanja ulikuwa sh. 2,861,000.

Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,144,400, TFF sh. 2,861,000, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 1,430,500, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) sh. 286,100 na asilimia 10 ya gharama za mechi ni sh. 2,861,000.

Gharama za awali za mechi ni nauli ya ndani kwa waamuzi sh. 10,000, nauli ya ndani kwa kamishna sh. 10,000, posho ya kujikimu kamishna sh. 40,000, posho ya kujikimu waamuzi sh. 120,000 na mwamuzi wa akiba sh. 30,000. Gharama za tiketi sh. 4,000,000, umeme sh. 300,000, usafi na ulinzi kwa uwanja sh. 2,350,000 na Wachina (Beijing Construction) sh. 2,000,000.

Gharama nyingine ni Jichangie ambayo ni sh. 200 kwa kila tiketi; kila klabu ilipata sh. 990,500 wakati DRFA ilipata sh. 849,000.
 FEBRUARI,12, 2012


WAAMUZI watatu na kamishna mmoja wameondolewa kuchezesha na kusimamia mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kutokana na kuonesha upungufu katika uchezeshaji na usimamizi.

Ofisa Habari  wa shirikisho la mpira wa miguu nchini (TFF) Boniface Wambura amesema uamuzi huo ulifanywa na Kamati ya Ligi iliyokutana jana (Februari 11 mwaka huu) ambapo pamoja na mambo mengine ilipitia taarifa za waamuzi na makamishna wa VPL ambayo leo (Februari 12 mwaka huu) inaendelea katika raundi ya 17.

PETER MUJAYA wa Mwanza aliyechezesha mechi namba 101 kati ya JKT Ruvu Stars na Yanga amefungiwa kwa miezi 12 kwa mujibu wa Kanuni ya 26(a) ya Ligi Kuu ya Vodacom kwa kushindwa kumudu mchezo huo, hivyo kupata alama za chini.

Naye ISIHAKA SHIRIKISHO wa Tanga ameondolewa kwenye orodha ya waamuzi wa VPL msimu huu kwa kushindwa kumudu mchezo namba 105 kati ya Simba na JKT Oljoro.
Moja ya udhaifu alioonesha ni kushindwa kumuadhibu mchezaji Patrick Mafisango ambaye alimsukuma baada ya kumuonesha kadi nyekundu Haruna Moshi wa Simba.

Mwamuzi mwingine aliyefungiwa kwa miezi 12 kwa mujibu wa Kanuni ya 26(a) ni KENNEDY MAPUNDA wa Dar es Salaam aliyechezesha mechi namba 107 kati ya Villa Squad na Simba.

Moja ya udhaifu wa Mapunda ni kushindwa kumpa kadi nyekundu Fred Cosmas wa Villa Squad baada ya kumuonesha kadi ya pili ya njano.

Pia waamuzi wasaidizi MICHAEL MKONGWA wa Iringa na KUDURA OMARY wa Tanga waliochezesha mechi namba 112 kati ya Yanga na Mtibwa Sugar wameondolewa katika mechi zilizobaki za VPL kwa kutokuwa makini.

Mwamuzi wa mechi hiyo Ibrahim Kidiwa amepewa onyo.

Waamuzi wengine waliopewa onyo na kutakiwa kujirekebisha ni Hashim Abdallah wa Dar es Salaam aliyechezesha mechi namba 92 kati ya Moro United na Yanga, na mwamuzi msaidizi wa mechi ya Simba na Coastal Union, Issa Malimali wa Ruvuma.

Kamishna wa mechi namba 112 kati ya Yanga na Mtibwa Sugar, Mohamed Nyange ameondolewa katika orodha ya makamishna kwa mechi zilizobaki za VPL kutokana na ripoti yake kuwa na upungufu.

Xxxxxxxxxxxxxxxxxx
KATIKA hatua nyingine kamati ya Ligi imeagiza mchezaji Patrick Mafisango wa Simba aandikiwe barua ya onyo kutokana na kumsukuma mwamuzi Isihaka Shirikisho baada ya kumuonesha kadi nyekundu mchezaji mwenzake Haruna Moshi kwenye mechi kati ya Simba na JKT Oljoro.

Nayo klabu ya Simba imepigwa faini ya sh. 500,000 baada ya washabiki wake kurusha makopo ya soda na chupa za maji wakipinga uamuzi wa mwamuzi Shirikisho kumtoa kwa kadi nyekundu Haruna Moshi.

Wachezaji waliopigwa faini ya sh. 500,000 kila mmoja baada ya kuoneshwa kadi nyekundu na ambao watakosa mechi tatu za ligi kwa mujibu wa Kanuni ya 25 ni nahodha wa Yanga, Shadrack Nsajigwa na Cyprian Lukindo wa Villa Squad.

Xxxxxxxxxxxxxx
Pambano la Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Simba na Azam lililochezwa Februari 11 mwaka huu katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam limeingiza sh. 67,548,000.

Jumla ya watazamaji 19,257 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo namba 117 kwa kiingilio cha sh. 3,000, sh. 5,000, sh. 10,000 na sh. 15,000 kwa VIP A.

Baada ya kuondoa gharama za awali za mchezo na asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni sh. 10,303,932.20 kila timu ilipata sh. 13,182,800.34, uwanja sh. 4,394,266.78.

Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,757,706.78, TFF sh. 4,394,266.78, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 2,197,133.39, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) sh. 439,426.78 na asilimia 10 ya gharama za mechi ni sh. 4,394,266.78.

Gharama za awali za mechi zilikuwa nauli ya ndani kwa waamuzi sh. 10,000, nauli ya ndani kwa kamishna wa mchezo sh. 10,000. wamuzi wa akiba sh. 30,000, tiketi sh. 4,350,000, maandalizi ya uwanja (pitch) sh. 400,000, umeme sh. 300,000, usafi na ulinzi kwa uwanja sh. 2,350,000 na Wachina (Beijing Construction) sh. 2,000,000.

Gharama nyingine ni Jichangie ambayo ni sh. 200 kwa kila tiketi; kila klabu ilipata sh. 1,347,990,280 wakati Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kilipata sh. 1,555,420.



FEBRUARI, 10, 2012
LIGI Kuu ya Vodacom (VPL) inaingia raundi ya 17 kesho (Februari 11 mwaka huu) kwa mechi tano huku ile ya Kagera Sugar na Mtibwa Sugar iliyokuwa ichezwe Februari 12 mwaka huu ikilazimika kusogezwa mbele kwa siku moja.

Mechi za kesho (Februari 11 mwaka huu) ambazo zitaanza saa 10 kamili jioni ni kati ya Simba na Azam (Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam), Toto Africans na Moro United (Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza), Polisi Dodoma na Villa Squad (Uwanja wa Jamhuri, Dodoma), Coastal Union na African Lyon (Uwanja wa Mkwakwani, Tanga) na JKT Oljoro na JKT Ruvu (Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha).

Kagera Sugar na Mtibwa Sugar sasa zitacheza Februari 13 mwaka huu kwa vile Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba siku ya Februari 12 mwaka huu umetolewa kwa shughuli za kijamii.
Mabadiliko hayo pia yamesababisha mechi kati ya Toto Africans na Mtibwa Sugar iliyokuwa ichezwe Februari 15 mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba sasa kuchezwa Februari 16 mwaka huu.

Nayo mechi namba 119 kati ya Yanga na Ruvu Shooting iliyokuwa ichezwe Februari 12 mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam- Chamazi, sasa itafanyika siku hiyo hiyo kwenye Uwanja wa Taifa.
Mechi hiyo imehamishiwa Uwanja wa Taifa kutokana na maombi ya Yanga kwa vile itakuwa ni sehemu ya sherehe za maadhimisho ya miaka 77 tangu kuasisiwa kwa klabu hiyo.
XXXXXXXXXXXXXXXXXX
MECHI ya Kundi A ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kati ya Mgambo Shooting ya Tanga na Morani ya Manyara iliyokuwa ichezwe Februari 11 mwaka huu kama ilivyokuwa ile ya Kundi C kati ya AFC ya Arusha na Polisi ya Morogoro zimesogezwa mbele kwa siku moja.
Mabadiliko hayo yametokana na mechi hizo kuingiliana na za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) zinazochezwa kwenye viwanja vya Mkwakwani, Tanga na Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha.

Mechi nyingine za FDL zitaendelea kesho (Februari 11 mwaka huu) kama ratiba inavyoonesha. Kundi A, Burkina Faso itakuwa mwenyeji wa Polisi Dar Salaam kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro wakati Temeke United na Transit Camp zitaoneshana kazi Uwanja wa Mabatini mjini Mlandizi.

Kundi B litashuhudia mechi kati ya Mbeya City na Majimaji kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya huku JKT Mlale wakiwa wenyeji wa Small Kids kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea. Nayo Tanzania Prisons itakuwa mgeni wa Polisi Iringa kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora.

Mechi ya Kundi C itakuwa moja ambapo Rhino FC itakaikaribisha 94 KJ ya Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.

XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
PAMBANO la Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Yanga na Mtibwa Sugar lililochezwa Februari 8 mwaka huu katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam limeingiza sh. 49,510,000.

Ofisa Habari Shirikisho la Mpira wa Miguu  nchini  (TFF) Boniface Wambura amesema jumla ya watazamaji 14,604 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo namba 112 kwa kiingilio cha sh. 3,000, sh. 5,000, sh. 10,000 na sh. 15,000 kwa VIP A.

Baada ya kuondoa gharama za awali za mchezo na asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni sh. 7,552,372.88 kila timu ilipata sh. 8,933,048.14, uwanja sh. 2,977,682.71.

Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,191,073.08, TFF sh. 2,977,682.71, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 1,488,841.36, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) sh. 297,768.27 na asilimia 10 ya gharama za mechi ni 2,977,682.71.

Gharama za awali za mechi zilikuwa nauli ya ndani kwa waamuzi sh. 10,000, nauli ya ndani kwa kamishna wa mchezo sh. 10,000.

Posho ya kujikimu kwa kamishna na waamuzi sh. 160,000, mwamuzi wa akiba sh. 30,000, tiketi sh. 4,000,000, maandalizi ya uwanja (pitch) sh. 400,000, umeme sh. 300,000, usafi na ulinzi kwa uwanja sh. 2,350,000 na Wachina (Beijing Construction) sh. 2,000,000.

Gharama nyingine ni Jichangie ambayo ni sh. 200 kwa kila tiketi; kila klabu ilipata sh. 1,022,280 wakati Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kilipata sh. 876,280.
 JANUARI 31, 2012

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeteua waamuzi kutoka Misri kuchezesha mechi ya kwanza ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za 29 za Kombe la Mataifa ya Afrika kati ya Tanzania na Msumbiji.

Waamuzi watakaochezesha mechi hiyo namba 25 itakayochezwa Februari 29 mwaka huu katika  Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam ni Farouk Mohamed atakayekuwa mwamuzi wa kati.

Wasaidizi wake ni Ayman Degaish na B.T Abo El Sadat wakati mwamuzi wa akiba ni Ghead Grisha.

Kamishna wa mechi hiyo ni Loed Mc Ian wa Afrika Kusini. Mchezo wa marudiano kwa ajili ya fainali hizo zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini utafanyika jijini Maputo baadaye mwaka huu.


Xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx 
NAHODHA wa timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya wanawake (Twiga Stars), Sophia Mwasikili ameondoka jana alfajiri (Januari 30 mwaka huu) kwa ndege ya Turkish Airlines kwenda Uturuki kucheza mpira wa kulipwa.

Ofisa Habari Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura amesema Mwasikili amekwenda kujiunga na Luleburgazgucu Spor Kulubu inayoshiriki Ligi Daraja la kwanza ya wanawake nchini humo.

Beki huyo wa kati wa Twiga Stars aliyekuwa akichezea timu ya Sayari Women amejiunga na klabu yake hiyo mpya kwa mkataba wa miaka miwili.

Awali Mwasikili alitakiwa kujiunga mapema na timu hiyo lakini alilazimika kusubiri kwanza mechi ya marudiano ya Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) kati ya Twiga Stars na Namibia (Brave Gladiators) iliyochezwa Januari 29 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Xxxxxxxxxxxxxxxxxxx
MECHI  ya marudiano ya raundi ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza fainali za nane za kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) kati ya Tanzania (Twiga Stars) na Namibia (Brave Gladiators) imeingiza sh. 38,220,000.

Kiasi hicho ni kutokana na watazamaji 16,334 waliokata tiketi kushuhudia mechi hiyo iliyochezwa juzi (Januari 29 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam na Twiga Stars kuibuka na ushindi wa mabao 5-2.

Viingilio katika mechi hiyo vilikuwa sh. 1,000 (watoto), sh. 2,000 (viti vya kijani na bluu), sh. 3,000 (viti vya rangi ya chungwa), sh. 5,000 (VIP C na B) na sh. 10,000 kwa VIP A.

Watoto waliokata tiketi kuingia uwanja ni 634, viti vya rangi ya kijani na bluu 13,238, viti vya rangi ya chungwa 1,040, VIP B na C 1,246 na VIP A watazamaji 176.

Wakati huo huo  Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) limewashukuru washabiki na wadau wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine kufanikisha mechi hiyo kati ya Twiga Stars na Namibia.

JANUARI 27, 2012
Mechi namba 100 ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya JKT Ruvu na Yanga itachezwa kesho (Januari 28 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, jijini  Dar es Salaam kwa mujibu wa ratiba ya ligi hiyo. Lakini mechi hiyo itaanza saa 12 kamili jioni badala ya saa 10 kamili jioni.

Ofisa habari shirikisho la mpira wa miguu nchini (TFF), Boniface Wambura amesema mabadiliko hayo ya muda yamefanyika ili kutoa nafasi kwa timu ya Taifa ya Namibia kufanya mazoezi kwenye uwanja huo saa 10 jioni kabla ya mechi yao ya Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) dhidi ya Twiga Stars itakayochezwa Jumapili (Januari 29 mwaka huu) kwenye uwanja huo kuanzia saa 10 kamili jioni.

Kwa mujibu wa kanuni za mashindano ya AWC yanayoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), siku moja kabla timu ngeni ni lazima ipewe fursa ya kufanya mazoezi kwenye uwanja utakaotumika kwa mechi katika muda ule ule.

Pia kutokana na mechi ya Twiga Stars na Namibia, mechi namba 102 kati ya Moro United na Azam iliyokuwa ichezwe Januari 29 mwaka huu katika uwanja wa Chamazi, jijini Dar es Salaam, sasa itachezwa Januari 30 mwaka huu kwenye uwanja huo huo.

Mabadiliko hayo hayajaathiri mechi nyingine za mzunguko wa 15. Mechi hizo ni kati ya Villa Squad na Toto African (Januari 28 mwaka huu- Uwanja wa Chamazi), Ruvu Shooting na Kagera Sugar (Januari 28 mwaka huu- Uwanja wa Mlandizi), Mtibwa Sugar na Coastal Union (Januari 29 mwaka huu- Uwanja wa Manungu), African Lyon na Polisi Dodoma (Februari 1 mwaka huu- Uwanja wa Chamazi) na Simba na JKT Oljoro (Februari 1 mwaka huu- Uwanja wa Taifa).

Viingilio kwa mechi za Uwanja wa Taifa ni sh. 3,000 viti vya bluu na kijani, sh. 5,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 10,000 VIP C na B, na sh. 15,000 VIP A wakati Uwanja wa Chamazi ni sh. 3,000 kwa mzunguko na sh. 10,000 kwa jukwaa.

Xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
WAAMUZI kutoka Ethiopia ndiyo watakaochezesha mechi namba 7 ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Yanga na Zamalek ya Misri itakayochezwa Februari 18 mwaka huu katika uwanja wa taifa, jijini Dar es Salaam.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limemteua Bamlack Tessema kuwa mwamuzi wa kati kwenye mechi hiyo wakati waamuzi wasaidizi ni Yilma Knife na Mussie Kindie.

Mwamuzi wa akiba atakuwa Waziri Sheha wa Tanzania na Kamishna wa mchezo huo ni Charles Kafatia wa Malawi.

Xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeandaa kozi ya ukocha ngazi pevu (advanced level) itakayofanyika Dar es Salaam kuanzia Februari 12 hadi 25 mwaka huu.

Wakufunzi ni kocha wa taifa stars, Jan Poulsen ambaye pia ni mkufunzi wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Sunday Kayuni ambaye pia ni mkufunzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na Kocha wa timu za Taifa za vijana Kim Poulsen ambaye pia ni mkufunzi wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Denmark (DBU).

Wambura amesema mwisho wa kupokea maombi kwa makocha wanaotaka kushiriki kozi hiyo ambayo ada yake ni sh. 60,000 itakuwa Februari 5 mwaka huu.

Sifa kwa waombaji ni elimu ya kuanzia kidato cha nne, wawe wanafanya kazi hiyo ya ukocha na wamefaulu vizuri mafunzo ya ukocha ngazi ya kati (intermediate level).

Pia wawe wamefundisha angalau kwa miaka miwili baada ya kupata cheti cha intermediate level.

Pia wanatakiwa maombi yao yawe yameidhinishwa na ama vyama vya makocha wa mpira wa miguu vya mikoa, vyama vya mpira wa miguu vya wilaya au vyama vya mpira wa miguu vya mikoa.

Kwa makocha watakaofaulu kozi hiyo watakuwa wamepata sifa ya kuhudhuria kocha ya ukocha ya Leseni C ya CAF.

JANUARI 26, 2012
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeteua waamuzi kutoka Burundi kuchezesha mechi ya Kombe la Shirikisho kati ya Simba ya Tanzania na Kiyovu Sport ya Rwanda itakayochezwa jijini Kigali.
Waamuzi hao ni Thierry Nkurinziza atakayekuwa katikati wakati wasaidizi wake ni Jean-Claude Birumushahu na Jean-Marie Hakizimana.
Mwamuzi wa akiba atakuwa Hudu Munyemana kutoka Rwanda. Kamishna wa mechi hiyo ni Abbas Sendyowa kutoka Uganda.
Mechi hiyo namba 13 itachezwa Februari 18 mwaka huu kwenye Uwanja wa Amahoro jijini Kigali, na itaanza saa 9.30 kwa saa za Rwanda. Mechi ya marudiano itachezwa Machi 4 mwaka huu,  katika uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam.
 Xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limemteua Leslie Liunda wa Tanzania kuwa Kamishna wa mechi namba 3 ya Ligi ya Mabingwa kati ya AS Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na Atletico Olympique ya Burundi itakayochezwa kati ya Februari 17, 18 na 19 mwaka huu jijini Kinshasa.
Waamuzi wa mechi hiyo ambao wanatoka Gabon watakuwa Mbourou Roponat, Wilfred Nziengu na David Obamba. Mwamuzi wa akiba kutoka DRC ni Mupemba Nkongolo.
Mechi ya marudiano kwa timu hizo itachezwa kati ya Machi 2, 3 na 4 jijini Bujumbura ambapo Kamishna atakuwa Eugene Katamban kutoka Uganda.
XXXXXXXXXXXXXXXXX
Tamasha la mafunzo ya kuhamasisha watoto kucheza mpira wa miguu na kuvumbua vipaji (Grassroot) kwa shule maalum zilizochaguliwa katika Mkoa wa Dar es Salaam linaendelea Februari 3 mwaka huu.
Ofisa Habari Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Boniface Wambura amesema siku hiyo tamasha hilo litafanyika katika Shule ya Msingi Mtoni Kijichi wilayani Temeke kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 6 mchana.
 Februari 10 mwaka huu tamasha lingine litafanyika katika Shule ya Msingi Kinyerezi wilayani Ilala.
Watoto (wa kike na kiume) wanaotakiwa kushiriki katika matamasha hayo ambayo yataendelea kila wiki katika shule mbalimbali za Dar es Salaam hadi Agosti 24 mwaka huu ni wa kuanzia umri wa miaka 6 hadi 12.
Matamasha hayo ni mwendelezo wa uzinduzi wa Grassroot katika tamasha (festival) kubwa lililofanyika Desemba 17 mwaka jana katika uwanja wa taifa, jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na watoto 1,200 baada ya semina iliyoendeshwa na Mkufunzi kutoka Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
Xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Mkuu wa mkoa wa Arusha Magesa Mulongo amesema kwa kushirikiana na wadau wa mpira wa miguu mkoani humo  watajitahidi kufufua timu zote zilizoshuka daraja ikiwa ni pamoja na kujua sababu za timu hiyo kushuka daraja ikiwamo timu ya mkoa wa arusha iliyokuwa inashiriki ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara ya Arusha Football Club (AFC).
 Akizungumza na wachezaji wa timu ya Jkt oljoro Mulongo amesema mkoa wa arusha ni mkubwa una sifa nzuri hivyo ni lazima idadi ya timu ziongezeke ikiwezekana zifikie nne ili kuendelea kuupa sifa mkoa huo.
 Amesema michezo ina wadau wengi lakini pindi wanaposhindwa kufanya vizuri inawakatisha tamaa na kupelekea wadau kuwekeza katika mambo mengine ya maendeleo.
 Pamoja na mambo mengine ameahidi kukutana na uongozi wa chama cha mpira wa miguu mkoani Arusha ili kujua sababu zilizopelekea timu ya AFC Arusha kufanya vibaya na kushuka daraja.

IDADI YA WASOMAJI

TUSIKILIZE LIVE KUPITIA TUNEIN

UNGANA NASI FACEBOOK HAPA

10 ZILIZOSOMWA ZAIDI

Labels